Watalamu wa sekta mtambuka Halmashauri za Arusha, Jiji la Arusha na Monduli, wametakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza mradi wa US- Aid Kizazi Hodari unaotekelezwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Kanda ya Kaskazini Mashariki unaolenga kuboresha Afya, Ustawi na Ulinzi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, vijana na walezi wanaotoka katika mazingira yaliyoathirika sana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.
Rai hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi, Mipango na Uratibu, Apolinary Seiya, kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Albano Musa, wakati akifungua kikao kazi cha kujadili mikakati ya kutekeleza mradi huo kwa mwaka 2025 pamoja na kujadili utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi kilichopita cha mwaka 2024 kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Amesema kuwa, Mkoa wa Arusha unaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha Ustawi wa watoto, vijana, familia pamoja na wananchi kwa ujumla wa Mkoa huo unaboreka zaidi.
Kwa upande wake Mkurugenzi mshiriki wa Asasi zinazotekeleza Mradi huo wa USAID Kizazi Hodari Kanda ya Kaskazini Mashariki, Aminiel Mongi amesema kuwa Mradi huo utatekelezwa kwenye Mikoa 9 na halmashauri 48 za Kanda ya Kaskazini Mashariki baada ya kuongezeka kwa halmashauri 8 ikiwemo Halmashauri ya Arusha ambazo hazikuwepo kwenye mradi huo.
Hata Hivyo, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Arusha, Dennis Mguye amesema kuwa ujio wa mradi huo ni hatua muhimu ya kuongeza nguvu kwa wasimamizi wa mashauri ngazi ya jamii kuibua watoto wenye waishio katika mazingira hatarishi na kuwapatia huduma.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Arusha Seleman Msumi ikiwa ni halmashauri iliyoingizwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, amesema kuwa halmashauri hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia, hivyo mradi huo utaongeza nguvu kwa pamoja kukomesha matukio ya kikatili.
Hata hivyo, mradi huo umekuwa na mafanikio makubwa kwa mwaka 2024 ambapo watu 7,154 walifikiwa na kupewa huduma sawa na 104% ya watu 6,872 ya watu waliopangwa kufikiwa na kupewa huduma.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.