Na Elinipa Lupembe
Jumla ya wanafunzi 29,508 mkoa wa Arusha, wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2024, unaoanza Novemba 11 - 29, 2024 nchini, kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania.
Akitoa taarifa ya kufanyika mtihani huo, Afisa Elimu Mkoa wa Arusha, Mwl. Sara Mlaki, amesema kuwa, kati ya watahiniwa hao 29,508, wasichana ni 16,222 na wavulana ni 13, 286.
Aidha, wanafunzi 28,209, wavulana ni 12,769 na wasichana 15,440, ni watahiniwa wa shule 'school candidates' watakaofanya mtihani kwenye shule 255 za Serikali na binafsi kukiwa na mikondo 760 huku Wanafunzi 1,299 wavulana 517 na wasichana 782,
ni watahiniwa wakujitegemea 'Private candidates' watakaofanya mtihani kwenye vituo 61 vilivyoanishwa vikiwa na mikondo 54.
Afisa Elimu Mlaki amebainisha kuwa, maandalizi yote yamekamilika ikiwemo uwepo wa vifaa vyote muhimu pamoja na wasimamizi wote kupatiwa semina elekezi, na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kwa kuhakikisha mahitaji yote muhimu ikiwemo rasilimali fedha kutolewa kwa wakati.
Hata hivyo Afisa Elimu huyo, amewasisitiza wasimamizi wote wa mtihani kuwa waadilifu kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na taratibu za mtihani wa Taifa na kuwaasa kutojihusisha na vitendo ambavyo ni kinyume na sheria na maadili ya utumishi wa Umaa, kwa kutambua kuwa kazi wanayoifanya ni kwa maslahi mapana ya watoto wakitanzania ambao wanategemewa kuwa ndio wajenzi wa Taifa lao
Sambamba na hilo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe Paul Christian Makonda @baba_keagan wanawatakia kila la kheri wahitimu wote waweze kufanya mtihani wao vyema na kufaulu vizuri pamoja na kuwakumbusha watahiniwa wote kuzingatia maelekezo na kujiepusha na aina yoyote ya vitendo vya udanganyifu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.