Wanunuaji wa Saruji Mkoa wa Arusha wametakiwa kudai risiti pindi wanapouziwa, ili kurahisisha ufuatiliaji kwa wafanyabiashara wanaouza Saruji kwa bei ya juu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Arusha.
“Arusha hakuna shida ya Saruji, isipokuwa kuna baadhi ya wafanyabiashara ndio wanafanya hali ya Saruji kuonekana kama ni shida kwa kupandisha bei kiholela,”alisema.
Amesema Saruji kwa Mkoa wa Arusha ipo yakutosha na inauzwa kwa bei halali hasa kwa wafanyabaishara wa jumla.
Changamoto kubwa ilijitokeza ni baadhi ya wafanyabaishara wa rejareja kupandisha bei ya Saruji kiolela ili wajipatie faida zaidi.
Kimanta amewataka wafanyabiashara wa Saruji kuhakikisha wanafuata bei zilizopangwa katika Mkoa wa Arusha na atakae kiuka hatua kali za kisheria zitafuatwa ikiwemo kufungiwa biashara yake.
Aidha, wafanyabiashara wa rejareja wametakiwa kuzingatia bei ya Saruji kwa mfuko mmoja usizidi 17,500 kwa Wilaya za Arusha,Arumeru, Longido, Karatu na Monduli na kwa Wilaya ya Ngorongoro bei kikomo itakuwa 22,500.
Kimanta amesema maelekezo hayo yanatakiwa kuanza mapema Novemba 18,2020.
Mkoa wa Arusha umefanya ukaguzi kwa wauzaji wa Saruji Jumla na rejareja kwa kufuata maelekezo yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa mapema Novemba 18,2020 Jijini Dodoma.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.