Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande amewataka washiriki kufanya kazi zao kwa weledi na kuzingatia maadili ya taaluma yao huku akiweka wazi kuwa, Wizara ya Fedha inaendelea kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wataalam wa Ununuzi na Ugavi.
Mhe Chande amesema hayo muda mfupi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe.Dkt. Doto Mashaka Biteko (Mb) Doto Biteko kufungua Kongamano la Watalamu wa Ununuzi na Ugavi, linalofanyika kwenye kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha, ukumbi wa Simba, leo Desemba 17,2024.
Mhe. Chande, amesema kuwa, miongoni mwa mambo yanayosababisha mkwamo Serikalini ni pamoja na wivu, choyo na fitna miongoni mwa watumishi, hivyo amewataka kuondokana na mambo hayo ili kukua na kujiletea maendeleo.
"Tumieni Taaluma yenu kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia kanuni sheria na taratibu za taaluma na utumishi wa Umma, msiogope kulaumia kwa kuzingatia sheria na taratibu za kazi na hakikisheni mnakuwa waadilifu, waaminifu na kuachana na tabia za wivu, choyo na husda tabia ambazo zinazua migongano kazini zenye chuki, jifunzeni kuwa wastahimilivu na kusamehe zaidi" Amesema
Amewasisitiza kutumia Taaluma zao kwa kuwa, Sheria ya Ununuzi wa Umma sura 410 inawalinda wataalam wa Ununuzi na Ugavi na kuwataka kutembea kifua mbele na kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Awali, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) Benezeth Ruta ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha zinazoiwezesha taaluma hiyo kusonga mbele.
Amesema Bodi hiyo inaendelea na utekelezaji wa Sheria Na. 23 ya mwaka 2007 kuhakikisha kuhakikisha Wataalam wanaofanya shughuli za ununuzi na ugavi wana sifa stahiki za kufanya kazi hizo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.