"Mkichanjwa wote mtawafanya watalii kutoka nje ya nchi wawe na amani na wengi watavutiwa kuja Tanzania hasa Mkoa wetu wa Arusha ambao ni kitovu cha Utalii".
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella alipokuwa akikagua zoezi la utoaji chanjo ya UVIKO 19 katika ofisi za chama Cha waendesha watalii Tanzania (TATO),Jijini Arusha.
Mtalii anapokuja Tanzania atapenda kuhudumiwa na watu waliochanjwa kuanzia Dereva hadi muongoza watalii, hivyo ni vizuri wadau wa sekta hii kuichukulia chanjo hii kama ni njia ya kurudisha hali nzuri ya Utalii Mkoani kwetu.
Amewataka Wakurugenzi wa makampuni ya Utalii kuwahamasisha wafanyakazi wao kupata chanjo ili iwe rahisi kwao kupata kazi nyingi kutoka kwa watalii hao.
Aidha, ameupongeza uongozi wa chama Cha waendesha watalii Tanzania (TATO) kwa kuwaimiza wanachama wao kupata chanjo ya UVIKO 19, na ameaidi Serikali kuendelea kushirikiana nao kwa kuhakikisha hali ya Utalii inarudi kama awali.
Nae, Mwenyekiti wa TATO bwana Wilbad Chambulo amesema wao kama wadau wa Utalii wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuchanjwa kwani hakuna mtalii kutoka nje atakaependa kufanyakazi na Mtanzania ambae hajachanjwa.
Amewasisitiza wanachama wa chama hicho hasa waliochanjwa kuwahamasisha wenzao ambao hawajachanjwa waweze kupata chanjo hiyo mapema kwani hali ya Utalii katika Mkoa wa Arusha imeanza kuimarika kidogo.
Mkurugenzi wa kampuni ya Serengeti Balloon Safari bwana John Course ameipongeza Serikali kupitia kwa Mhe Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kukubali watanzania wachanjwe chanjo ya UVIKO 19.
Anasema ilikuwa ni kilio chao cha muda mrefu, na sasa Serikali imeweza kukitimiza na wanauhakika sasa utalii utarudi kwenye hali yake ya awali.
Amewasihi watanzania kutoogopa kupata chanjo hiyo kwani ni salama kabisa na itaiweka huru nchi yetu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha Dkt. Silvia Mamkwe amesema bado watu wanatakiwa kujitokeza kwa hiari kupata chanjo ya UVIKO 19 kwani ili nchi iweze kuwa huru na janga hili inaitaji kuwa na watu waliochanjwa kati ya 60% hadi 80%.
Amesema kwa Mkoa wa Arusha jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika kuhakikisha watu wengi wanachanjwa na moja ya njia ya kuhamasisha ni kuwa na gari litakalopita katika Mitaa mbalimbali ili kutoa chanjo hiyo kwa wale ambao watashindwa kufika katika vituo husika.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.