Watanzania watakiwa kuwa na utamaduni wakunywa maziwa kila siku ili kujenga afya za miili yao na kuongeza pato la taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mkuu wa Wilaya ya Arusha Daniel Daqarro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo,amesema katika kuadhimisha wiki ya maziwa Mkoani Arusha, wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi katika viwanja vya Themi Njiro maalufu kama viwanja vya nanenane.
Amesema maonyesho hayo ya wiki ya maziwa yanatija kubwa sana kwa wafugaji,wasindikaji na wananchi kwa ujumla kwani wataweza kujifunza juu ya umuhimu wa unywaji maziwa na ufugaji wa kisasa.
Aidha,amewataka maafisa mifigo wote kuhakikisha wanasambaza elimu hiyo mpaka ngazi za chini kwenye jamii hususani namna ya ufugaji wa Ngo’mbe wachache na wenye tija.
Mwenyekiti wa bodi ya maziwa bwana Charles Malunde, amesema unywaji wa maziwa kwa Mtanzania mmoja ni wastani wa lita 47 kwa mwaka ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki ambapo wastani upo juu,hasa nchi ya Kenya ni lita 63 kwa Mwaka.
Amesema maziwa ni mlo kamili kwani yamebeba virutubisho vya aina zote vinavyoitajika katika mwili wa binadamu.
Akisisitiza zaidi,amesema Tanzania ina takribani Ng’ombe milioni 30.5 ambapo Ngo’mbe milioni 27 niwakienyeji na wanatoa lita 1 hadi 1.5 ya maziwa kwa siku na milioni 1 ndio Ngo’mbe wa kisasa.
Tanzania ina idadi kubwa ya Ngo’mbe na hawana tija katika uzalishaji wa maziwa kwani Ngo’mbe wa kisasa wanauwezo wakutoa lita 30 hadi 40 za maziwa kwa siku.
Kaimu Mkurugenzi wa balaza la Kilimo Tanzania bwana Timothy Mbaga,amesema maonyesho hayo ya 21 hayatakuwa na kiingilio chochote ili kutoa fursa zaidi kwa wafugaji kushiriki kwa wingi.
Pia maonyesho hayo yatawasaidia wafugaji kupata maarifa mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na takribani makapuni 40 yameshathibitisha ushiriki.
Maonyesho ya mifugo na wiki ya maziwa Kitaifa yatafanyika jijini Arusha kuanzia Mei 30 hadi Juni 1, 2018 katika viwanja vya Themi Njiro na yatafunguliwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Luhanga Mpina na kufungwa na Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Selemani Jafo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.