Serikali itasimamia mipango yote itakayotumika kupinga na kutokomeza ukatili wa kijinsia hasa kwa watoto wa kike kwa kuhakikisha taarifa zao zinafanyiwa kazi kwa haraka zaidi.
Yamesemwa hayo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Kimanta alipokuwa akizindua siku 16 za maadhimisho ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia Kimkoa,Jiji la Arusha.
“Maadhimisho haya yanatakiwa kuleta mabadiliko katika jamii zetu kwa kupunguza ukatili huu kwa wanawake na watoto, na ili haya yote yaweze kufanikiwa ni lazima kila mmoja wetu awe tayari kuelimisha jamii yake.”
Amesema kwa takwimu za mwaka 2019 hadi 2020 jumla ya wanawake 1302 wamefanyiwa ukatili wakinjinsia na watoto 1256, ambapo wakiume walikuwa 171 na wakike 1,085 na kwa mwaka 2018 hadi 2019 waliofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa watoto walikuwa 988, hii ni ongezeko la asilimia 22 kulinganisha na mwaka 2020.
Aidha, amewataka watoto wasiwe waoga wa kutoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili wa kijinsia.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wakupinga ukatili wa kijinsia Mkoani Arusha, Mkurungezi mkazi kutoka shirika la World Education inc. (WEI) BI. Lilian Badi,amesema katika mradi wao watawapa nafasi wahanga wa unyanyasaji wa kijinsia kutoa elimu katika jamii.
Bi.Lilian amesema shirika lake litaendeleo kutoa elimu katika maeneo mbalimbali ya jamii hasa katika kipindi hiki cha maadhimisho ya siku 16, ili jamii ipate uwelewa zaidi wa namna ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia.
Maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia Mkoani Arusha yamezinduliwa leo yakiwa yamebeba kauli mbiu isemayo “Tupinge Ukatili wa Kijinsia: Mabadiliko Yanaanza na Mimi" na yatafanyika kwa siku 16 kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.