Na Elinipa Lupembe
Watumishi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wameanza kupatiwa Mafunzo ya Mfumo wa Upimaji Utendaji kazi kwa watumishi wa Umma (PEPMIS), yanayofanyika kwenye ukumbi wa mikutano, Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha, na kutolewa chini ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Rasilimali Watu kwa kuhirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala mkoa.
Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi Utumishi na Rasilimali watu, Davia Lyamongi, kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Arusha, amewataka watumishi hao, kufanya bidii kipindi cha mafunzo ili kupata ujuzi na maarifa ya namna ya kutumia Mfumo huo wa PEPMIS.
Amesema kuwa mfumo huo, utawezesha upimaji wa kazi alizopangiwa mtumishi kwa siku, kulingana na majukumu aliyopangiwa na muda wa kufikia malengo pamoja na tathmini na upimaji.
"Kila mtumishi anapaswa kuuelewa vizuri mfumo huu, kwa kuwa unamgusa moja kwa moja utendaji wake wa kazi, kwa kuzingatia malengo binafsi na kufikia malengo ya jumla ya Mwajiri ambaye ni Serikali, niwasisitize nafasi hii ni muhimu kwa kila mtumishi, kuhakikisha unauelewa vizuri mfumo huu mpya wa PEPMIS" Amesema Lyamonge
Naye Msimamizi Mkuu wa mafunzo kutoka Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Anna Kiwelu, amesema, mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi, yenye lengo la kumuwezesha mtumishi wa Umma, kujifanyia upimaji wa kazi anazozitekeleza kila siku kupitia mfumo wa PEPIMS.
Amebainisha kuwa, lengo la mafunzo hayo, ni kuwajengea uwezo watumishi na kuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya kutumia mfumo wa PEPIMS, ambao ni mfumo mpya uliotolewa na serikali kwa ajili ya kupima utendaji kazi kwa watumishi wote wa Umma.
Mafunzo hayo ya siki mbili, yamejumuisha watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha, Ofisi za Wakuu wa Wilaya pamoja na Ofidi za Maafisa Tarafa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.