Na Elinipa Lupembe
Wawekezaji wa Kampuni ya Hanspaul inayomiliki Kiwanda cha kutengeneza na kuunganisha magari maalum kwa ajili ya shughuli za Utalii mkoani Arusha, wameipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwa na Sera bora zinazovutia wadau kuwekeza nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Hanspaul, Satbir Singh Hanspaul kiwandani hapo, hakusita kuipongeza Serikali, kwa kuwa na Sera nzuri zinazosababisha mazingira rafiki kwa wawekezaji kufanya kazi za uzalishaji nchini.
Ameweka wazi kuwa, kupitia Kituo cha Uwekezaji cha Taifa, imeweka mazingira rafiki yanayowezesha wawekezaji wa ndani kufanyakazi kwa kushirikiana na sekta zote, zaidi mazingira yanayoruhusu na kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi kuwekeza Tanzania.
"Kiwanda chetu tunatengeneza magari yanayotumia umeme na yameanza kutumiwa na watalii, tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Tamthilia ya Royal Tour imeleta watalii wengi nchini, watalii ambao baaadhi yao wanavutiwa kuwekeza Tanzania, huku TIC ikifanyakazi kubwa ya kuwaunganisha wafanyabiashara wakubwa, makampuni na watu binafsi".Amesema Satbir Singh
Hata hivyo amesema kuwa kutokana na amani na utulivu wa kijamii, kiuchumi na kisiasa nchini, umewezesha watanzania na wageni kutoka nje ya nchi kufanya shughuli za uzalishaji mali kwa uhuru, unaokwenda sambamba na kukuza uchumi wa nchi.
Awali, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa Ndani, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Felix John amesema kuwa, TIC inafanya kampeni ya kitaifa kwenye mikoa ya Kanda ya Kaskazini ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, ikiwa na lengo la kutoa elimu kuhusu zana ya uwekezajia pamoja ja kubadili fikra na mtazamo wa watanzania kwamba wawekezaji ni wageni kutoka nje ya nchi.
"Kampeni hiyo ni muhimu kwa watanzania, inayolenga pia kuwahamasisha watanzania, kushiriki kikamilifu kwa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kiuchumi na kuchangamkia fursa zilizoko" Amebainisha John
Hata hivyo, ameaeka wazi kuwa, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, kwa kushirikiana na TIC, wameshusha kiwango cha fedha za uwekezaji hasa kwa wazawa kutoka Dola za Kimarekani 100,000 hadi kufikia 50,000 sawa na Sh.milioni 125, kwa lengo la kuwavutiwa wawekezaji wa ndani kuwekeza na kusajili miradi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.