Na Elinipa Lupembe
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amesisitiza dhamira ya Serikali ya awamu ya sita ya kuendelea kuutangaza Utalii wa Tanzania Duniani kote, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya watalii wanaokuja kutembelea vivutio vya Utalii vinavyopatikana Tanzania.
Mhe. Kairuki ameweka wazi dhamira hiyo ya Serikali, wakati akizindua Msimu wa 9 wa Maonesho ya Karibu-Kili Fair 2024 yanayoendela kwenye Viwanja vya Magereza Mjini Arusha, Juni 07, 2024 huku akisisitiza Serikali kutambua mchango wa sekta binafsi katika jitihada za kuukuza na kuutangaza utalii nchini.
Waziri Kairuki amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuutangaza utalii kupitia programu ya Tanzania The Royal Tour na Amaizing Tanzania, programu ambazo zinaendelea kufanya vizuri katika kuchagiza sekta ya Utalii kwa kuongeza idadi ya watalii wanaofika kutalii Tanzania.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa utalii wakiwemo Mawakala wa Usafiri, wamiliki wa Makampuni ya Utalii ili kuhakikisha wanawejengewa uwezo na wanakuwa sehemu ya Mabalozi wa Utalii wenye kubeba jukumu kubwa la kuutangaza utalii wa Tanzania Duniani kote.
Hata hivyo, Mhe. Kairuki ameishukuru Kampuni ya Kili Fair Promotion Ltd kwa kuandaa Maonesho hayo ya Karibu - Kili Fair 2024, maonesho ambayo yanachangia na kuvutia watalii kuja Tanzania huku yakichangia ongezeko kubwa la idadi ya watalii wanaofika nchini Tanzania pamoja na kuifahamisha Dunia kuhusu vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania.
#ArushanaUtalii
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.