Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameeleza kuwa, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27,2024 utakuwa wa haki, uwazi.
Pia, uchaguzi huo utazingatia misingi ya umoja na mshikamano, pamoja na falsafa ya R4 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Waziri Mchengerwa amesema kuwa, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilianzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kusogeza maamuzi karibu kabisa na wananchi.
Amefafanua kwa kusema kwamba, uchaguzi wa serikali za mitaa ni tofauti na uchaguzi mkuu, kwani mfumo wake unalenga wakazi ambao wanatambuana katika maeneo yao.
Utambuzi huu wa wakazi unategemea wenyewe wakazi wa eneo husika.
Amesema hayo Novemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini.
Waziri Mchengerwa ameendelea kusema kwamba Bunge halikufanya marekebisho ya Ibara ya 145 na 146 ya katiba, wala tafsiri ya sheria inayosimamia uchaguzi wa serikali za mitaa.
Hata hivyo, Bunge lilifanya marekebisho ya sheria inayosimamia mchakato wa chaguzi zinazoratibiwa na Tume Huru ya Uchaguzi.
Vilevile Waziri Mchengerwa ameeleza kwamba, kumekuwa na propaganda za kisiasa kuhusu hali ya uchaguzi wa serikali za mitaa, ambapo amedai zinatolewa na baadhi ya watu ambao hawakuwa wamejiandaa vyema.
Amesema kuwa, uchaguzi huo ni shirikishi, na maandalizi yamehusisha vyama vyote vya siasa kwa njia ya vikao na mashauriano ya mara kwa mara na wadau wa vyama vya siasa.
Kuhusu kutotumika kwa vitambulisho wakati wa uandikishaji, Waziri Mchengerwa amesema
"Tungeweza kunyima haki za Watanzania walio wengi endapo tungeamua kuwa lazima kila mtu awe na kitambulisho ili aandikishwe.
"Tunatambua kwamba wananchi wengi, hasa wanaoishi kwenye vitongoji na vijiji, hawana vitambulisho.
"Hivyo, hatua hii imezingatiwa ili kila Mtanzania apate fursa ya kushiriki uchaguzi," amesema Mheshimiwa Mchengerwa.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.