Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa @mohamed_mchengerwa ameahidi Serikali kutoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kata ya Mundarara wilaya ya Longido mkoa wa Arusha.
Mhe. Mchengerwa ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Mundarara kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Mundarara Septemba 18, 2024, kufuatia ombi la wananchi hao kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma kituo cha afya katika eneo lao, unaotokana na idadi kubwa ya watu wanajishughulisha na uchimbaji wa madini.
Amesema kuwa lengo la Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kufikishia kwa wananchi huduma zote muhimu ikiwemo huduma za afya, elimu, miundombinu ya umeme, barabara na maji na kusisitiza kuwa Serikali itatoa fedha na ujenzi utaanza mara moja.
"Niwaahidi wananchi wa Mundarara, Serikali itatoa shilingi milioni 300 na Kituo cha afya kitajengwa hapa Mundarara, Rais wetu anayo nia dhati ya kuhakikisha kila mtanzania anafaidi matunda ya nchi yake, huduma zote za msingi ni haki ya kila mtanzania". Amesema
Hata hivyo ameahidi kutoa milioni 125 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Longido - Mundarara na daraja la Matiani na kuuiagiza Uongozi wa TARURA mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na TARURA wilaya ya Longido kuanza mara moja ujenzi wa daraja hilo, linalounganisha kata hiyo ya Mundarara na kata nyingine, daraja ambalo lilibomoka wakati wa msimu wa mvua za mwaka huu na kusababisha adha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo.
"Ninawaagiza TARURA anzeni mara moja ujenzi wa daraja hilo ili wananchi wapate huduma ya usafiri kwa haraka , eneo hili ni muhimu sana kutokana na shughuli za uzalishaji wa madini pamoja na muingiliano mkubwa wa kibiashara, hivyo wananchi hawatakiwi kukwama kutokana na miundombinu ya barabara, tengenezeni daraja ili huduma hiyo irejee kama awali". Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi mkoani humo.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.