Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaagiza wakuu mikoa yote ya pembezoni mwa nchi, kuimarisha zaidi ulinzi na usalama wa mipakani ili kujilinda na Homa ya Nyani 'Mpox' kuweza kuingia nchini.
Mhe. Mchengerwa ametoa maagizo hayo leo Jumatano Septemba 18, 2024 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, wakati wa ziara yake ya kikazi Wilayani Longido Mkoani Arusha akitahadharisha kuchukua hatua kwa Mamlaka za Wilaya na Mikoa itakayozembea na kusababisha ugonjwa huo kuingia nchini Tanzania.
"Ugonjwa huu hauko mbali,upo jirani tu kwahiyo msingi huu wa kuimarisha ulinzi katika mipaka yetu itatusaidia kutambua yule anayeingia lazima afanyiwe uchunguzi wa kiafya kwa mujibu wa namna taratibu za wenzetu wizara ya afya walivyotupatia." Amesema Mhe. Mchengerwa.
Mhe. Mchengerwa kadhalika ameahidi kuzungumza na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba katika kuhakikisha kuwa kunafungwa mashine za ukaguzi kwenye kituo cha Namanga kinachounganisha Arusha na Nchi jirani ya Kenya ili kudhibiti vinavyoingia nchini Tanzania kupitia mpaka huo.
Katika hatua nyingine wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Longido, Mhe. Mchengerwa amemsifu Mhe. Makonda kwa ubunifu, kujiongeza kwake na namna ambavyo ameendelea kujitoa kwa nguvu zake zote katika kuhakikisha ustawi wa wananchi wa mkoa wa Arusha pamoja na kutekeleza kikamilifu ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.