WAZIRI MKUU: “TUMIENI MATOKEO YA TAFITI ZA KISAYANSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA KITAIFA"
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Idara na Taasisi za utafiti na elimu ya juu kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingirana kutumia matokeo ya tafiti hizo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Kitaifa.
Mhe. Majaliwa amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Afya Moja uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) Arusha leo Novemba 4, 2024.
Amesema, Taasisi zote zinazohusika na masuala mtambuka katika afya ya jamii, wanyama na mazingira zitenge fedha na kuweka katika mipango ya Taasisi hizo afua za kuthibiti magonjwa ya kizoonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, magonjwa yasiyoambukiza, mabadiliko ya tabia nchi na usalama wa chakula.
“Wizara za kisekta, na Mamlaka za Serikali za Mitaa, andaeni mipango kazi na taratibu za usimamizi kwa ajili ya utekezaji wa mbinu ya Afya Moja kwa kuzingatia miongozo iliyopo ambayo imeweka bayana majukumu ya wadau wote Pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa fanyeni vikao vya mara kwa mara, kufanya tathmini ya utekelezaji wa pamoja wa afua mbalimbali, kwa kufanya hivyo changamoto zitajulikana mapema na kupatiwa ufumbuzi” Amesema.
Aidha amesema kuwa, tafiti zinaonesha duniani kote takribani visa bilioni moja vya ugonjwa pamoja na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na zaidi ya asilimia 75 ya vimelea vipya 30 vya magonjwa vilivyogunduliwa katika miongo mitatu iliyopita, vimetoka kwa wanyama.
“kwa mujibu wa taarifa na takwimu zilizopo, Taifa la Tanzania kama mataifa mengine duniani limekuwa likikumbwa na magonjwa hayo, Kama mtakumbuka, mnamo mwaka 2017 wataalam wetu kutoka sekta mbalimbali waliainisha magonjwa ya zoonotiki yanayopewa kipaumbele hapa nchini ambayo ni kichaa cha mbwa; kimeta; malale; brusela; homa ya bonde la ufa; homa ya mafua; na magonjwa yanayosababishwa na virusi vya ebola na Marburg” Ameeleza Waziri Mkuu,
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.