Na Elinipa Lupembe
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi amemuagiza Afisa Elimu Mkoa wa Arusha kuharakisha mchakato wa usajili wa shule mpya tarajali ya Msingi Lucas Mhina iliyopo katika Kijiji cha Losirwa wilayani Monduli mkoani Arusha, ili shule ipate fursa ya kupokea wanafunzi wa kuanza masomo kwa mwaka wa masomo unaoanza Januari 2024.
Mhe Ndejembi ametoa agizo wakati wa hafla ya uzinduzi wa shule hiyo, ambayo tayari miundombinu yake imekamilika, ikiwa imesheheni vyumba kutosha vya madarasa, ofisi za walimu, vyoo pamoja na samani za madarasa
Aidha amemuagiza mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Monduli,
kuwapanga walimu wa kwenye shule hiyo kabla ya Januari 2024 ili kipindi chote cha uandikishaji wanafunzi walimu wawepo shuleni hapo.
“Nimpongeze sana, Lucas Mhina kwa uzalendo wake wa kutafuta wafadhili ambao wamejenga shule hii nzuri kwa ajili ya kusaidia watoto wa jamii ya wafugaji ili waweze kupata elimu karibu na maeneo wanayoishi na kiwasaidia kuondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwani sasa shule imeletwa karibu" Amesema Naibu Waziri
Ameomgeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini kazi zinazofanywa na wadau wa maendeleo na inaunga mkono juhudi hizi hivyo nimuagize Afisa Elimu Mkoa kuhakikisha anaharakisha shule hii iweze kupata usajili ili iweze kuanza kupokea wanafunzi watakaojiunga Januari 2024
Aidha Mhe Naibu Waziri Ndejembi ametoa rai kwa wananchi wa kijiji cha Losirwa kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu ya shule hiyo ili kuleta tija kwa wanafunzi watakaoanza masomo hapo.
Kwa upande wake, Mfadhili wa shule hiyo, Lucas Mhina amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoifungua Nchi kiuchumi na hivyo kuwawezesha wahisani mbalimbali kuja nchini kuwekeza na kusaidia miradi ya maendeleo huku akiahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuwaletea watanzania maendeleo.
Mhina ameikabidhi shule hiyo kwa Serikali ambapo tayari vyumba 20 vya madarasa , Ofisi ya Walimu, matundu 14 ya vyoo vya wanafunzi, matundu manne ya vyoo vya walimu, nyumba mbili za walimuj zimejengwa pamoja na kuwekwa madawati 100, matanki mawili ya maji pamoja na kisima cha maji.
#ArushaFursaLukuki
#KaziInaendelea
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.