WAZIRI wa Afya @ummymwalimu ametoa onyo kwa baadhi ya wahudumu wa afya wanaouza dawa za Amoxicillin DT kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakati wanapoenda kupatiwa matibabu ambapo dawa hizo kwa maelekezo ya Serikali hutolewa bure.
Waziri Ummy ametoa agizo hilo mkoani Tanga wakati akikabidhi gari ya kubebea wagonjwa 'Ambulance' katika kituo cha afya Duga kilichopo Jiji la Tanga ambapo amebainisha kuwa gari hilo ni miongoni mwa Magari zaidi ya 600 yanayosambazwa nchi zima na wizara ya afya kwa kushirikiana na ofisi ya Rais tawala za mikoa na Serikali za mitaa 'TAMISEMI' lengo likiwa ni kutokomeza vifo vya wagonjwa wakiwemo wajawazito wanapohitaji huduma za dharura.
"Lengo letu ni kuboresha huduma za rufaa kwa wagonjwa tunataka tusipoteze watu kwa sababu wagonjwa walikuwa wanafariki kwa sababu ya kukosa huduma kwa wakati hususani wagonjwa wa dharura"
Akizungumzia changamoto ya dawa zinazouzwa kinyume na maelekezo ya Serikali , Waziri Ummy amewataka wahudumu wa afya kuzingatia sera ya afya bure kwa wamama wajawazito na watoto.
"Kama dawa zipo hamna haja ya kumwambia mgonjwa changia zingatieni sera ya matibabu kwa wamama wajawazito na watoto waliopo chini ya miaka mitano , nimeangalia daftari la wagonjwa kati ya 10 watoto waliokuja hospital 7 wana maambukizi ya Bakteria ambayo inatibiwa na dawa inaitwa Amoxicillini DT.
"Dawa hii ya a Amoxicillin DT haipaswi kuuzwa kwa watoto waliopo chini ya miaka mitano na hili nalisisitiza tuzingatie maelekezo ya Serikali , kwa sababu tumeona inauzwa mwaka huu tutaandika haiuzwi sasa ole wake tuikute kwenye Duka inauzwa utatuambia umeitoa wapi"
Katika kulidhibiti hilo waziri Ummy amesema watatoa semina elekezi kwa viongozi kuanzia ngazi za vijiji na vitongoji ili kutokomeza tabia hiyo ya baadhi ya watoa huduma ikiwemo maduka ya dawa kuuza dawa ambazo Serikali imeelekeza zitolewa bure kwa wagonjwa.
"Itabidi tuende mpaka ndani tuweke alama utakapoonoa hii dawa imeandikwa GOT ukiiona jua kuwa imeibiwa na haipaswi kuuzwa hizi dawa zinanunuliwa na Serikali na kusambaza hii ndio sera ya matibabu bure"
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.