Mkuu wa Mkoa wa Arusha mheshimiwa Idd Hassan Kimanta amemtaka mganga mkuu wa Jiji la Arusha Daktari Kheri Kagya, kuhakikisha anaweka mazingira yaliyo bora na rafiki kwa wazee wanapoenda kupata matibabu katika vituo vya afya.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi wa baraza la wazee wa jiji la Arusha,katika ukumbi wa shule ya Arusha School.
“Wazee hawatakiwi kuhangaika katika kupata huduma mbalimbali hasa za matibabu, bali watumishi ndio wanapaswa kuhakikisha wanawahudumia kwa haraka zaidi,alisema”.
Amesema wazee ni hazina katika ujenzi wa maendeleo ya Mkoa kwa kutoa ushauri mbalimbali kadri ya uzoefu walio nao.
Mwenyekiti wa baraza la wazee wa Jiji la Arusha bwana Mhina Sezua amesema, wamefurahi sana kukutana na Mkuu wa Mkoa na kuaidi kutoa ushirikiano mkubwa katika uongozi wake.
Aidha, amesema kazi kubwa ya wazee ni kushauri tu pale wanapoona inaitajika kufanya hivyo ili kuleta maendeleo ya Mkoa kwa ujumla.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya viongozi wa wazee hao bi. Fauster Licky amesema, kweli wazee wamefurahishwa sana na kiongozi mkubwa kama Mkuu wa Mkoa kukutana nao na kusikiliza changamoto zao.
Amesema hiyo inaonesha ni kwa namna gani uongozi wa Mkoa unavyowathamini wazee na kuwachukulia kama ni moja ya nguzo za maendeleo ya Mkoa.
Mheshimiwa Kimanta amekutana na viongozi wa baraza la wazee wa Jiji la Arusha kwa niaba ya wazee wote kwa lengo la kujitambulisha kwao na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.