Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Dkt. Athumani Kihamia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Karatu bwana Rajabu Kalia kuhakikisha wanaweka miundombinu ya TEHAMA ya ukusanyaji mapato katika Hospitali ya Wilaya ya Karatu.
Ameyasema hayo alipokuwa akikagua ujenzi wa Hospitali hiyo na kuwataka waanze mapema kuweka mifumo hiyo wakati ujenzi unaendelea ili huduma zitakapoanza zitumie mfumo huo wa ukusanyaji mapato.
"Mkichelewa kuweka mfumo huo na huduma zikaanza mtapoteza mapato mengi sana ni bora viende sambamba vyote sasa hivi", alisema.
Aidha, Dkt. Kihamia amesisitiza kuongezwa kwa kasi ya ujenzi wa Hospitali hiyo ili waweze kukamilisha baadhi ya majengo ambayo bado kama vile jengo la utawala na maabara.
Amewataka wakasimamie kwa ukaribu zaidi kwa kushirikiana na wakuu wa idara kwani Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 1.7 ikiwa ni kutoka Serikali kuu na Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.
Mwenyekiti wa halmshauri ya Karatu Mhe. John Mahu amesema kukamilika kwa Hospitali hiyo kutasaidia huduma za Afya kusogea karibu kwa wananchi na kupunguza hadha ya wagonjwa wengi kupelekwa mbali.
Ameaidi kwenda kushirikiana na madiwani wengine wa Halmashauri hiyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa haraka.
Dkt. Kihamia amefanya ziara ya siku moja ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu baada ya kasi ya ujenzi kuwa ndogo na hivyo kupelekea kutokamilika kwa wakati.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.