Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta amewataka wadau wa maji katika Mkoa wa Arusha kuweka wazi taarifa zao za kiutendaji ili kutoa nafasi ya utatuzi wa changamoto kwa urahisi.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa maji wa Mkoa wa Arusha, kikao hicho kilichojumuisha sekta za umma na binafsi.
Kimanta amesema uwazi wa taarifa utarahisisha kila mdau kuwa na uwelewa wa pamoja wa kila sehemu na kurahisha kupata suluhu ya changamoto.
Amesema mpaka sasa hali ya upatikanaji maji katika Mkoa wa Arusha hasa vijijini bado ipo chini sana kwani Mkoa ulijiwekea malengo ya kusambaza maji vijijini kwa 85% ifikapo 2020, lakini mpaka sasa ni 69.5% ya upatikanaji wa maji vijijini ndio umetekelezwa kuanzia 2015-2020.
Vijiji 304 ndivyo vimeshapata maji hadi kufikia mwaka 2020 na vijiji 86 bado havijapatiwa maji kati ya vijiji 390 vyote na serikali inaendelea kuongeza wigo wa upatikanaji wa maji katika vijiji hivyo.
Kimanta amesema bado malengo ya serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 Mkoa wa Arusha uwe umefikia 100% ya upatikanaji maji vijijini.
Amesisitiza kuwa changamoto ya maji niya kila mmoja hivyo amewataka wadau hao kuhakikisha wanatoka na mpango mkakati mkubwa wa kuwezesha wananchi kupata maji kwa haraka zaidi.
Akitoa taarifa ya upatikanaji wa maji kwa Mkoa wa Arusha Meneja wa wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini injinia Emmanuel Makaidi amesema, RUWASA imependekeza bajeti ya Bilioni 17 kwa mwaka 2020/2021 na mpaka Februari 2021 bilioni 7.4 sawa na 58.7% zimeshatumika.
Makaidi amesema mpaka sasa RUWASA Mkoa wa Arusha imeshatekeleza miradi 4 yenye thamani ya bilioni 4.6 na miradi 8 inatarajiwa kuanzishwa katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Arusha.
Akitoa neno katika kikao hicho mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha bwana Zeloth Steven amesema ni vizuri sheria ya maji ikafahamika kwa mapana na kina kwa wananchi ili kuwaongezea uwelewa.
Aidha amewataka wadau hao wa maji kuhakikisha wana simamia miradi yote ya maji kwa umakini sana kwani katika kampeni za mwaka 2020 kero kubwa kwa wananchi ilikuwa ni upatikanaji wa maji katika maeneo mengi.
RUWASA Mkoa wa Arusha umefanya kikao chake cha kwanza cha wadau kwa lengo la kujitambulisha kwa wadau na kuweza kushirikiana katika mambo mbalimbali na wadau hao na kuweza kutatua changamoto zinazowakabili.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.