KATIBU Tawala mkoa wa Arusha,Dkt Athuman Kihamia ,amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya meru kuhakikisha ifikapo Julai 30,2022 ujenzi wa zahanati ya Kikatiti uwe umekamilika na kuanza kutoa huduma.
Kihamia ametoa maagizo hayo wakati alipotembea na kujionea ujenzi wa hospitali hiyo ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 80.
''Nawaagiza wajumbe wa kamati ya ujenzi wa zahanati hiyo ifikapo tarehe 30 julai mwaka huu ujenzi uwe umekamilika na wananchi waanze kupata huduma."
Kihamia amesema pia amemtaka Mganga mkuu wa halmashauri ya Meru kuhakikisha anashirikiana na watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia miundombinu ya halmashauri ili iweze kutoa tija kwa wananchi.
Kwa upande mwingine,Katibu Tawala amesema Serikali mkoani Arusha itaendelea kuchukua hatua kwa watumishi ambao watakwenda kinyume na sheria kwenye ufujaji wa fedha za umma watachukuliwa hatua kali za kisheria.
''Tutaendelea kuchukua hatua kali,msifikili kama hatua tulizochukua jiji la Arusha itaishia huko,hapana tutaendelea kuchukua hatua kote,na hatujaanzia jiji peke tumeanzia sehemu nyingi''Amesema Kihamia".
Kwa upande wake Mganga mkuu wa Halmashauri ya Meru, Dkt Maneno Matawa,amesema wameyapokea maelekezo ya Katibu tawala na kuhaidi kuyafanyia kazi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.