Wakulima, Wavuvi na Wafugaji wametakiwa kuzalisha mazao yenye tija yatakayo ongeza upatikanaji wa chakula kwa wananchi na kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba alipokuwa akifungua maonesho ya 27 ya Kilimo na sherehe za nanenane kanda ya Kaskazini katika viwanja vya Themi Njiro jijini Arusha.
“Sekta ya Kilimo ina umuhimu mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi kwani ni sekta inayoajiri watanzania zaidi ya asilimia 75”,alisema Mgumba.
Amesema ni jukumu la kila mkulima,mvuvi na mfugaji kuhakikisha anazalisha kwa wingi mazao mbalimbali kwa kutumia elimu na teknolojia watakazozipata katika maonesho hayo.
Hata hivyo, serikali ya awamu ya tano bado imeweka nguvu kubwa katika sekta hizo kwa kurudisha serikalini mashamba ya Basutu yaliyopo Mkoani Arusha ili yagawiwe kwa wananchi kwa lengo la kuendeleza Kilimo.
Pia, serikali imejenga vihenge vya kuhifadhi chakula kinachonunuliwa na serikali, na kuruhusu ndege takribani 4 zitakazotumika katika kusafirisha mazao ya Maua, Matunda na Mbogamboga katika nchi za Ulaya na Uarabuni, hii yote itaongeza ukuwaji wa soko la uhakika katika sekta hiyo.
Amewataka wakulima, wavuvi na wafugaji kusambaza elimu hiyo watakayoipata katika maonesho hayo hadi kwa wakulima wa ngazi ya kata na vijiji katika kukuza sekta hiyo.
Akitoa neno la ukaribisho Mkuu wa Mkoa wa Arusha Idd Hassan Kimanta amesema, maonesho hayo hayatakuwa na tija ikiwa kama hayataleta mabadiliko katika sekta hizo za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji.
Hivyo, amesisitiza tathimini ifanyike mapema ili iweze kutoa mwelekeo mapema wa maonesho hayo kwa baadae na mabadiliko kwa ujumla.
Mwenyekiti wa kamati ndogo ya maandalizi Bwana Richard Kwitega amesema, jumla ya waoneshaji 350 wameshajiandikisha katika maonesho ya mwaka 2020 na wanatarajia idadi kuongezeka zaidi.
Maonesho ya sherehe za nanenane kwa kanda ya Kaskazini yanafanyika kwa mara ya 27 na Kitaifa yanafanyika katika viwanja vya Nyakabimbi Mkoani Simiyu na kilele chake kinatarajia kuwa Agosti 10,2020.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.