Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Arif Abbas Manji na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda wamekubaliana kushirikiana pamoja katika kuvutia watalii na wawekezaji mbalimbali kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya Utalii mkoani Arusha na Visiwani Zanzibar kwa kutumia vyema maonesho ya utalii na Uwekezaji yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar Oktoba 25-26 ya mwaka huu.
Mashirikiano hayo ya pamoja yamefikiwa leo Jumamosi Oktoba 05, 2024 wakati Viongozi wa Kamisheni hiyo walipofika Mkoani Arusha kukutana na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Viongozi wa waongoza watalii Mkoani hapa, lengo likiwa ni kuwaalika kushiriki kwenye Maonesho hayo ya kwanza ya kimataifa, yatakayofanyika kwenye kituo cha Maonesho Dimani.
Arusha ni Mkoa kinara kwa Utalii wa Tanzania bara, ukitajwa kuiingizia nchi fedha nyingi zaidi za Kigeni huku idadi ya watalii ikiongezeka zaidi tangu kuchezwa kwa Filamu ya The Royal Tour iliyoongozwa na Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan huku Zanzibar ikisifika kwa utalii wa fukwe barani Afrika, utalii ambao unachangia zaidi ya asilimia 30 kwenye pato la Taifa na takribani asilimia 80 ya fedha za kigeni.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.