Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Philip Isdor Mpango amewataka Mawakili na Wanasheria kusimamia maadili ya taaluma yao ili waweze kutenda haki.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa chama cha wanasheria Tanganyika, Jijini Arusha.
" Taaluma hii ni kama zilivyo taaluma nyingine hivyo mkishindwa kufuata maadili haki za wananchi zitapotea".
Aidha, amekitaka chama hicho kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote ambao watabainika wamekiuka sheria za taaluma hiyo ili iwe fundisho kwa wengine na haki iweze kupatikana kwa wananchi wote.
Vilevile, amekitaka chama hicho kuendelea kuongeza nguvu za kutoa elimu kwa wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwa kuwa wananchi wengi wanapoteza haki zao kwa kutokufahamu sheria.
Dkt. Mpango amewashauri mawakili kuangalia namna ya kupunguza gharama zakusikiliza mashauri kwa kushirikiana na mahakama ili wananchi waweze kumudu gharama hizo nakupata haki zao.
Amesema Serikali itaendelea kushirikiana na chama hicho na taasisi nyingine za kisheria ili kuhakikisha haki inapatikana maana ni msingi wa amani katika nchi.
Nae, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damasi Ndumbaro amesema Jamii iliyokosa haki siku zote haina amani, hivyo kazi ya sheria ni kusimamia haki na wanaotafsiri sheria hizo ni wanasheria.
Kwa upande wake, Rais wa chama cha mawakili Tanganyika Prof. Edward Hosea amesema chama hicho kimeweza kutoa msaada wa kisheria bure kwa wananchi takribani 7307.
Pia, chama hicho kimeongeza ushirikiano na Serikali katika kuishauri Serikali kwenye sheria ambazo zinaitaji maboresho na mchakato wa katiba mpya.
Akitoa salama za ukaribisho Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema wanasheria wanafanya kazi kubwa katika maswala ya sheria hasa kwa wananchi.
Mkutano Mkuu wa wanasheria ulianza Mei 8 na utaendelea kwa muda wa wiki nzima huku ukiambatana na semina mbalimbali kwa wanasheria hao.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.