Na Elinipa Lupembe
Hayawi hayawi hatimaye yamekuwa, ile ahadi aliyoitoa Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango kwa wananchi wa Tarafa ya Ketumbeine, ya kuwapa gari la wagonjwa wa dharura (ambulance) leo imetimia.
Dkt. Mpango ametimiza ahadi hiyo aliyoitoa, kufuatia ombi la wananchi wa Ketumbeine, wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Longido ya kuzindua Kituo cha Afya Ketumbeine Februari 10, 2024.
Wakizungumza wakati wa kukabidhiwa gari hilo, na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Loy Thomas Ole Sabaya, wananchi hao wameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali na kuwapa kipaumbele, miradi mingi ya maendeleo ikitekelezwa kwenye maeneo yao, ikiwemo kituo hicho kioya cha Afya.
Diwani wa kata ya KetumbeineMhe. Timotheo Menyoriti Laizer, licha ya kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwajengea kituo hicho cha afya, haikutosha na kuwaletea gari la wagonjwa, ambalo litaenda kuondoa vifo visivyo vya lazima kwa wakazi wa Ketumbeine, hususani vifo vya kinamama wajawazito na watoto, ambao walikuwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha kwa kucheleweshwa kupata huduma.
"Kipekee tunamshukuru Dkt. Mpango kwa kutimiza ahadi yake kwa wakati, inatupa mwanga ni kiongozi wa kipekee anayethamini watu, pia tunamshukuru Mama Samia kwa kuwajali wananchi wake, kwa kipindi kifupi cha uongozi wake Ketumbeine tumepata miradi mingi ya maendeleo, miradi ambayo imepunguza kero na changamoto nyingi za wananchi, ambapo hapo awali walikuwa kama wametengwa" Mhe. Menyoriti.
Naye, Noa Keiyan Mollell mkazi wa Ketumbeine, amemshukuru pia Mhe. Rais na kusema kuwa hapo awali, walitumia punda kubeba wagonjwa pindi wanapozidiwa lakini sasa wamepata gari, jambo ambalo, wanaiona Serikali ya Mama Samia ni ya tofauti sana, inayowajali na kuwapenda sana wananchi wake.
Mariam Laizer, amesema hatujawahi kuona maendeleo ya kasi hii, tunamshukuru mama Samia kwa kuwajali wanawake wa Ketumbeine, kwa kuleta huduma ya upasuaji kwenye kituo cha afya, zamani walilazimika kwenda Longido kufanyiwa upasuaji lakini sasa huduma zote zinapatikana kituoni hapo.
"Tunamshukuru mama Samia, wajawazito walipoteza watoto na wengine walipoteza maisha kwa kuchelewa kupata huduma, kwa kutupa gari hili, mama ametuletea uzima, ametuponya maumivu yote ya kupoteza ndugu zetu kwa kukosa huduma" Amesema Mariam
Hata hivyo Mganga Mkuu wa wilaya ya Longido, Dkt. Methew Majan, amesema kuwa, uwepo wa gari la wagonjwa kituoni hapo, utarahisisha usafiri pindi wanapotokea wagonjwa wa dharura, kwa kuwa hapo awali walilazimika kusubiri gari kutoka hospitali ya wilaya zaidi ya Km 55.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa