Balozi wa Ethiopia Nchini Tanzania Mhe.Shibru Mamo Kedida leo tarehe 28/08/2023 amefanya ziara Mkoani Arusha na kupokelewa na Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasimali Watu Bwana.David F.Lyamongi.
Katika mazungumzo hayo Mhe.Balozi Kedida ameomba Ushirikiano wa Kidugu Kati ya Jiji la Arusha na Jiji la Adis Ababa kutokana na kufanana kwa shughuli zake Kuu zikiwemo uwepo wa Taasisi za Kimataifa pamoja kuhodhi Mikutano mikubwa ya Kimaifa katika Majiji haya mawili Barani Afrika.
Sambamba na hilo,Mhe.Balozi Kedida amesema Ethiopia inaendelea kuimarisha usafiri wa Anga na Nchi ya Tanzania hususan Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na hivyo kuwataka Wafanyabishara mbalimbali kuendelea kutumia usafiri huo.
Aidha,Mhe.Balozi Kedida amesema Ethiopia inatambua mashirikiano baina Nchi mbili hizi na kuuomba Uongozi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kushirikiana kwa karibu na Jamii ya Waethiopia waishio na kufanya kazi katika Taasisi mbalimbali za Kimataifa na biashara hapa Arusha.
Kwa upande wake,Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Rasimali Watu Bwana.David F.Lyamongi amemhakikishia Mhe.Balozi Kedida kuwa Serikali ya Mkoa Arusha inatambua Ushirikiano wa Kidugu uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia na kuwa Jamii ya Waethiopia waishio Arusha wapo mikono salama na endapo wakiwa na jambo lolote la kuhitaji msaada Ofisi ya Mkuu wa Mkoa iko tayari wakati wowote kuwasaidia.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa