Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ikiambatana na Naibu Waziri wa Nishati Mhe.Judith Kapinga na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Mhandisi Gissima Nyamohanga , wametembelea kituo cha kupoza na kusafirisha Umeme cha Lemuguru, Mkoani Arusha Machi 13,2024.
Akizungumza kituoni hapo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mathayo David Mathayo (MB) amesema, Kituo hicho ambacho kitaziunganisha nchi za Tanzania na Kenya (Tanzania and Kenya Power inter connector), kitakua ni fursa ya kibiashara kati ya Tanzania na Kenya ,ambapo Tanzania itaweza kuiuzia umeme Kenya na Nchi nyingine zaidi ya 15, watakaokuwa wanahitaji Umeme
“Kupitia hiki kituo tutaweza kuwauzia umeme Nchi nyingine ,kwani hiki kituo kinatuunganisha na gridi za umeme za Nchi nyingine kupitia south Africa power pool na East Africa Power pool, baada ya mradi wa Bwawa la Julius Nyerere kukamilika tutakua na umeme wa kutosha na hivyo tutaweza kuwauzia Nchi zingine watakapohitaji” alisema Mhe.Mathayo
Aidha ameitaka TANESCO kukamilisha mradi huo ambao mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 99.6
Naye Naibu Waziri wa Nishati Mhe.Judith Kapinga ameishukuru kamati kwa kutembelea kituo hicho na kusema kuwa Ushauri uliotolewa na kamati utazingatiwa
“ Niishukuru kamati hii, na kusema kuwa tumepokea maelekezo na ushauri wao ikiwa ni kukamilisha mradi huu kwa asilimia ndogo iliyobaki ili kufanya mradi huu kuwa na Tija, alisema Mhe.Kapinga.
Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa kituo hicho takribani dola milioni 258
“Tunamshukuru Rais wetu Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwajili ya Miradi ya Nishati na hasa katika kituo hiki ambacho kitakua fursa ya Biashara ya Nishati ya Umeme kwa upande wa Nchi za kusini na Kaskazini, alisema Mhe.Kapinga
Aidha Mhe.Kapinga amesema kuwa kazi ya Wizara ya Nishati ni kusimamia miradi hii, ili fedha za Serikali zitumike ipasavyo kama ilivyokusudiwa.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa