Na Elinipa Lupembe
Kamati ya Siasa mkoa wa Arusha, imetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Masusu kata ya Pinyinyi wilaya ya Ngorongoro, na kuwapongeza wananchi wa kijiji hicho cha Masusu kwa ushirili wa ujenzi wa shule hiyo mpya katika kata yao, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 -2025.
Wajumbe hao wa Kamati ya Siasa wameridhishwa na kuwapongeza viongozi na wananchi wa Masusu kwa usimamizi imara uliwezesha mradi huo kutekelezwa kwa viwango, licha ya kuwa umechelewa kukamilika kutokana na eneo hilo kukabiliwa na uhaba wa maji.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Loy Thomas Ole Sabaya, amewapongeza wananchi wa eneo hilo, kwa kujitoa kushiriki ujenzi wa shule hiyo mpya kwa kuchangia nguvu kazi, na kuhakikisha shule hiyo inakamilika na watoto wanaanza masomo shuleni hapo.
"Tunawapongeza sana wananchi wa Masusu kwa juhudi zenu za kuiunga mkono Serikali yenu, hii inathibitisha namna mnamuunga mkono Mhe. Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Chama cha Mapinduzi, endeleeni na moyo huo wa kizalendo " Amesema Mwenyekiti Sabaya.
Nao wananchi wa Masusu, wamemshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwajengea shule katika kata yao, jambo ambalo wamekiri kuwafanya nao, kujihisi kama watanzania wengine, shule ambayo inatawasaidia watoto wao kupunguza mwendo wa kutembea zaidi ya Km 18 kwenda shule ya Sekondari jirani ya Sale.
Lazaro Selebu, mkazi wa Masusu, licha ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita, amethibitisha kuwa, kwa muda mrefu walitamani kuwa na shule kama ilivyo kwa kata nyingine na sasa serikali imetimiza kiu yao, wakishukuru watoto wa Masusu sasa kusoma karibu na nyumbani.
"Watoto wetu walilazimika kusoma mbali na nyumbani jambo ambalo lilitulazimu kutumiangharama kubwa na zaidi liliwatesa na kuwakatisha tamaa na baadhi ya watoto kuacha masomo kutokana na umbali, kwa sasa tuna uhakikisa watoto wetu kusoma na kufikia ndoto zao" Amesema Mosses Mollel
Akiwasilisha taarifa ya mradi huo mkuu wa shule mama ya Sekondari Sale, Mwl. Ngunai Gidore amesema kuwa, mradi huo wa shule mpya ya sekondari Masusu umetekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 584.2 Fedha kutoka Serikali Kuu kupitia program ya SEQUIP.
Mwl. Gidore amefafanua kuwa, katika ujenzi huo wananchi wa Masusu walichangia nguvu kazi ikiwa ni pamoja na kusafisha eneo la ujenzi, kuchimba msingi wa majengo yote pamoja na kusaidia kupakia mchanga na mawe uliotumika kutekeleza mradi huo.
Kiasi hicho cha fedha kimehusisha ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na Ofisi mbili, Jengo la Utawala, Maabara za Fizikia, Baiolojia na Kemia, Jengo la TEHAMA, Kichomea taka, tanki la kuhifadhia maji pamoja na vyoo vya wasichana, wavulana na wenye mahitaji maalum.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa