Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta ametoa maagizo kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kuhakikisha wanafanya kazi zao za usajili kwa kushirikiana na vyombo vya ulizi na Usalama.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua semina kwa ajili ya viongozi wa Wilaya na Mkoa wa Arusha,kuhusu usajili wa Vizazi kwa Watoto wa umri chini ya miaka 5.
Amesema zoezi hilo la usajili wa vyeti vya kuzaliwa linaitaji umakini na kuweka mbele uzalendo zaidi kwa maslahi ya Taifa na kuwezesha kusajili watoto wanaotakiwa tu.
Kimanta amesisitiza zaidi juu ya umuhimu wa usajili wa Watoto hao kwani itasaidia kuwa na takwimu sahihi na kuondokana na dhana ya kutumia takwimu za makisio.
Nae, Kaimu Mtendaji wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini Bi. Emmy Hadson amesema, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 Mkoa wa Arusha ulikuwa na jumla ya Watoto 310,887 na waliosajiliwa ni 23% tu.
Bi. Emmy amesema kupitia kampeni hii wanayotarajia kaianzisha katika Mkoa wa Arusha, itafavyika kwa wiki 2 na kisha zitatolewa siku 90 za kuhakikisha Watoto wenye umri chini ya miaka 5 wanasajiliwa bure.
Kwa watakaopoteza vyeti hivyo watatakiwa kulipia gharama ya shilingi 5000 kwa ajili ya kupatiwa cheti kipya.
Aidha, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha bwana David Lyamongi amesema, katika kampeni hii hamasa kubwa inaitajika ili kuweza kuwafikia wananchi wengi na wakajitokeza kwa wingi.
Amesisitiza kuwa katika usajili huu ni maandalizi ya kizazi kijacho hivyo umakini unaitajika ili kuhakikisha Watoto wanaoandikishwa ni wanaostahili.
Kampeni ya kusajili Watoto wenye umri chini ya miaka 5 tayari imeshafanyika katika Mikoa 18 na inaendelea katika Mikoa mingine ikiwepo Mkoa wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa