Na Elinipa Lupembe.
Wananchi wa kata ya Seela Sing'isi halmashauri ya Meru, wamemshukuru na kuipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Jemedari Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwajali na kuona umuhimu wa kuwapa mamilioni ya fedha ya kujenga shule mpya ya sekondari katika kata yao.
Wakizungumza shuleni hapo, wananchi hoa, ambao ni timu ya usimamizi wa mradi na wazazi waliofika kuchukua fomu za kujiunga kidato cha kwanza, hawakusita kuonesha hisia zao, juu ya mapenzi mema na uzalendo alionao mama Samia, kwa watanzania hususani wananchi wa Sing'isi na Arumeru kwa ujumla wake.
Elieneza Philipo Kitomari, licha ya kumpongeza Mhe. Rais, amekiri uwepo wa mapinduzi ya kasi kubwa ya maendeleo katika Serikali ya awamu ya sita, tofauti na awali na kuthibitisha kushuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa huku miradi ya mamilioni ya fedha ikitekelezwa kwenye maeneo ya vijijini kama ilivyo kwa kata yao ya Seela Sing'isi.
Amesema kuwa, katika umri wake ni mara ya kwanza kushuhudia, Serikali ikitoa fedha za kujenga shule nzima kwa wakati mmoja kwa maeneo karibu yote nchini, zenye miundombinu yote muhimu, kuanzia msingi mpaka kukamilika, huku wananchi, wakishirikishwa katika usimamizi, amekiri kuwa, hayo ni mahaba na mapinduzi ambayo hayakuwahi kufanyika hapo awali.
"Hii shule ni ya kata ukiangalia miundombinu yake haina tofauti na shule za 'private' tena imezidi, madarasa ya kisasa, maabara za masomo yote ya Sayansi, ujenzi umeanza na kukamilika kwa wakati, tayari walimu wamepangiwa na vitabu vimeletwa, sijawahi kushuhudia katika maisha na umri wangu huu, mama anagusa mioyo ya watanzania, tunaahidi kumuunga mkono kwa nguvu zote" Amekiri Kitomari
Naye, Neema Mbise, mzazi aliyefika kuchukua fomu ya kujiunga mtoto wake na kidato cha kwanza, ameipongeza serikali ya mama Samia na kusema kuwa mama amewakosha watanzania kwa kuhakikisha watoto wao wanasoma karibu na nyumbani.
"Mama anatupa raha, yaani anatukosha watanzania, tumezoea kuona majengo machafu machafu ya shule za serikali, leo hii majengo yanang'ara, yanajengwa mapya, ya zamani yanakarabatiwa, kifupi tunamuombea mama yetu, Mwenyenzi Mungu ambariki na amjalie afya njema" Amesema Neema.
Naye Kaimu Mkuu wa shule sekondari Madiira, Mwl. Joel Sidael Goroi, amesema kuwa miundombinu muhimu ya shule hiyo imeshakamilika na tayari 70% ya wazazi wameshachukua fomu za kujiunga watoto wao, ambapo wanafunzi 100 wamepangiwa shuleni hapo, wavulana 50 na wasichana 50.
Shule mpya sekondari Madiira imejengwa na Serikali kupitia programu ya kuboresha miundombinu ya Elimu Sekondari (SEQUIP) kwa gharama ya shilingi milioni 584, ikiwa imekamilika tayari kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 08 Januari, 2024.
#arushafursalukuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa