"Serikali haipingi mila na desturi bali haitafumbia macho zile mila na desturi zinazoleta ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto".
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa katika kilele cha siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, Jijini Arusha.
Matukio ya ukatili wa wanawake na watoto bado yapo sana katika Mkoa wa Arusha kwani kwa mwaka 2021/2022 jumla ya matukio 4705 yalilipotiwa na kati yake matukio 4013 yalikuwa ya wanawake na 692 ni wanaume na ndani yake yakiwepo ya watoto.
Katika mwaka 2019 jumla ya matukio 2339 yalilipotiwa ikiwa ni pungufu ya yale ya mwaka 2022 ambayo yalikuwa 4706 na hii imetokana na watu kupata uelewa wa kitoa taarifa juu ya matendo hayo ya ukatili.
" Naziagiza kamati za MTAKUWA kuanzia ngazi ya vijiji hadi halmashauri zifanye kazi na kila halmashauri ianzishe kituo cha Mkono kwa Mkono kwenye hospitali za Wilaya ili kuhakikisha vitendo vya ukatili vinatokomezwa', alisema.
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Arusha, Denis Mgiye amesema vitendo vya ukali vinavyoongoza ni ukatili wa kimwili,kisaikolojia,kingono, mimba na ndoa za utotoni, ukeketaji na kushindwa kutoa malezi kwa watoto.
Hata hivyo, amewahasa wanaume kujitokeza kwa wingi kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwani wameonekana wapo nyuma wakati vitendo vya ukali wanafanyiwa.
Nae, Afisa ustawi wa jamii kutoka kituo cha Mkono kwa Mkono cha hospitali ya Mt.Meru Daniel Kasikiwe amesema wahanga wengi wamejitokeza kutoa taarifa za ukatili na hiyo imewezekana baada ya elimu kuendelea kuwafikia wananchi.
Aidha, amesema bado kuna changamoto ya wahanga kuchelewa kutoa taarifa ndani ya masaa 72 na hivyo kusababisha kupotea kwa ushahidi na baadhi ya wahanga kutotoa ushahidi pindi kesi inapofika mahakamani.
Maadhimisho ya kupinga ukatili wa kijinsia na watoto yalianza Novemba 27 na yamemalizika Disemba 10 katika Mkoa wa Arusha ambapo utoaji wa elimu ulifanyika katika kila halmashauri kwa kupita kwenye mashule, vyuo na makundi mbalimbali ya wananchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa