Na Elinipa Lupembe.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Pascal Katambi Patrobass (Mb), ameridhishwa na hali ya utoaji na upatikanaji wa huduma kwa wasafiri wanaopitia mpaka wa Tanzania na Kenya kupitia Kituo cha Huduma za pamoja Mpakani (OSBP), eneo la Namang na kuwapongeza watendaji wa kituo hicho chenye ofisi za Taasisi 18 muhimu, ambazo ni maalum kwa kuwahudumia wasafiri wanaovuka mpaka huo.
Mhe. Katambi amesema hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja ya kukagua na kujionea hali halisi ya utendaji kazi na utoaji huduma katika mpaka huo kwa wasafiri, mali na mizigo yao pamoja na magari ya mizigo na kupongeza namna Serikali imeweka mifumo rahisi ya kudhibiti upitaji wa abiria na mizigo lakini kuwarahisishia wasafiri upatikanaji wa vibali vya kuvuka katika eneo moja.
Amesema kuwa, licha ya Kituo cha pamoja kuwa na mifumo inayowarahisishia abiria kupita mpakani, lakini amewataka wataalam kuzingatia hali ya usalama katika mipaka kwa kufanya upekuzi wa abiria na mizigo yao pamoja na magari ya mizigo kwa umakini na kujiridhisha, raia wanaovuka mpaka huo wanavyo vibali vyote halali ili kuzuia uhamiaji haramu na upitishaji wa bidhaa za magendo.
"Nimejionea Mifumo bora ya kuhudumia wasafiri inayodhibiti watu kupita bila vibali muhimu, ninaona uwepo wa miundombinu rafiki yenye mifumo ya kisasa, unaruhusu kila abiria kukaguliwa na kulipia na kupata vibali vyote katika eneo moja pamoja na kudhibiti usafirishaji haramu wa mali na binadamu, kituo ambacho kina hadhi ya kimataifa, ni ngumu sana mhalifu kupita hapa" Ameweka wazi Mhe. Katambi
Naye Mfawidhi wa Uhamiaji mpaka wa Namanga, Mrakibu wa Uhamiaji Bulugu Edward Mkanga, amesema kuwa, kituo hicho kinazo ofisi 18 za taasisi zinazohusika na usafiri wa mpakani na kuongeza kuwa makubaliano ya 'communique' yanayoruhusu raia wa nchi hizo mbili kutembea hadi Km 20 kwa pande zote umepunguza uhalifu na kuongeza muingiliano wa amani wa kijamii na kibiashara katika eneo la Tanzania.
"Kupitia 'communigue' raia wa Kenya anaruhusiwa kuingia hadi kipenyo cha Km 20 katika eneo la Tanzania kadhalika na raia wa Tanzania anaruhusiwa kuingi Kenya kipenyo hichohicho bila ya kuwa na kibali chochote, zaidi ni kitambulisho cha utaifa tu, jambo ambalo limefanikiwa kuongeza muingiliano wa kibiashara mpakani huku Tanzania ikinufaika kutoka na raia wengi wa Kenya kupenda kufika kuja eneo la Tanzania hasa nyakati za weekend kupata huduma za burudani" Amesema Mkaribu wa Uhamiaji Mkanga.
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Longido, Mhe. Marco Ng'umbi, amesema kuwa, hali ya usalama wilayani hapo ni shwari huku wakazi wake wakiendelea na shughuli zao za kila siku za kujitafutia kapato kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi, licha ya makubaliano ya muingiliano huo wa kipenyo cha kuingia hadi Km 20 kwa raia wa mpakani kwa pande zote mbili.
"Wilaya ya Longido inaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kusimamia matumizi ya mifumo inayotumika kwenye kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani (OSBP) Namanga, na kuhakikisha raia wanaoingia na kutoka nchini wanafuata taratibu zote, huku kukiwa na utaraibu imara na thabiti wa ukaguzi wa magari madogo na magari ya mzigo kabla ya kuvuka na kuingia nchini" Amefafanua Mhe. Ng'umbi
#arushafursaluki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa