_Asema uwekezaji wao umeongeza fursa za ajira na Mapato ya serikali_
_Waitangaza Tanzania kupitia Masoko yao ya Asia, Marekani na Ulaya__
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumatatu Septemba 29, 2025 ametembelea Viwanda vya A to Z na Sunflag Mkoani Arusha, akiwapongeza kwa uzalishaji wa bidhaa bora pamoja na kutoa fursa za ajira kwa wananchi wengi wa Arusha na hivyo kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na wa Mkoa wa Arusha kwa ujumla.
Mhe. Makalla ameeleza pia kufurahishwa na namna ambavyo Viwanda hivyo vimekuwa mabalozi wazuri wa Tanzania, kwa kuzalisha bidhaa ambazo zimekuwa zikiuzwa ndani na nje ya Tanzania pamoja na kusaidia katika uongezaji wa thamani ya mazao ya kilimo nchini ikiwemo zao la Pamba kutoka Mwanza linalotumika katika utengenezaji wa mavazi kwenye Kiwanda cha Sunflag kilichopo Njiro.
"Nimefika kwenu kwasababu ninyi ni walipaji wazuri wa kodi kwenye rekodi zetu, la pili mmeajiri watu wengi mkiisaidia serikali katika uzalishaji wa ajira kwa Watanzania na Jingine mnaitangaza nchi yetu kwa bidhaa mnazozitengeneza kwenye masoko ya ndani na nje ya Tanzania." Amesisitiza CPA Makalla wakati akizungumza na uongozi na menejimenti ya Viwanda hivyo.
Kulingana na Uongozi wa Viwanda hivyo Kiwanda cha A to Z kimeajiri zaidi ya Watanzania 8,000 huku Sunflag ikiwa imeajiri wafanyakazi 2700 kati yao 43 wakiwa Raia wa Kigeni, wakizalisha Mavazi mbalimbali pamoja na bidhaa za Plastiki na vifungashio mbalimbali ambapo Mhe. Makalla ameahidi kuendelea kushirikiana nao katika kutimiza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anayehimiza na kufanya jitihada za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira bora ya wafanyabiashara na Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuweza kufanya biashara zao katika mazingira mazuri na yaliyo salama.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa