Mtendaji Mkuu wa Leopard Foundation inayomilikiwa na Kampuni Mama ya Leopard Tour inayojishughulisha na masuala ya Utalii Mkoani Arusha, Ndugu Zuher Fazal leo Ijumaa Januari 24, 2025 kwaniaba ya Taasisi hiyo, amekabidhi Pikipiki 20 kwa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha katika jitihada za kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama Mkoani Arusha.
Wakati wa makabidhiano hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda, Ndugu Fazal amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa usimamizi wake mzuri wa sekta ya utalii nchini, akisema kuimarika kwa Sekta hiyo pamoja na mafanikio makubwa yanayopatikana chini ya Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ndicho kilichowahamasisha kujitoa kuchangia Vitendetakazi hivyo kwa Jeshi la Polisi.
Kwa Upande wake Mhe. Makonda,licha ya kuishukuru Leopard Foundation, ameahidi kuendelea kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha kwaniaba ya Mhe. Rais Samia ili wafanyabiashara hao waendelee kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Arusha kupitia fursa mbalimbali za ajira wanazozizalisha pamoja na mchango wao wanaourudisha kwenye Jamii.
Leopard Foundation inayotoa usaidizi wa Kijamii katika mapambano dhidi ya umaskini pamoja na kusaidia katika elimu, usimamizi wa mazingira na afya, imeingia makubaliano pia na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika kusaidia huduma za matibabu kwa wahitaji wasiojiweza kiuchumi wanaofika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa kwaajili ya matibabu.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa