Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda leo Jumanne Disemba 17, 2024 mbele ya Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Mashaka Biteko, amewapongeza wananchi wa Kata ya Muriet Jijini Arusha, kwa maamuzi yao ya kumburuza Diwani wa kata yao kwenye matope kama sehemu ya kuonesha kukerwa na ubovu wa barabara za Muriet.
Wakati wa Kongamano la 15 la wataalam wa Ununuzi na Ugavi kwenye kituo cha Mikutano cha AICC lililofunguliwa mapema leo na Naibu Waziri Mkuu Dkt. Doto Biteko, Mhe. Makonda ameagiza kuzomewa kwa Viongozi wazembe wakiwemo madiwani, wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji pamoja na wabunge wanaoshindwa kutimiza majukumu yao, akikemea majungu na siasa zisizo na tija kwa wananchi.
Mhe. Makonda amesema Serikali kuu imetoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maendeleo Mkoani Arusha, badala yake mivutano imekuwa sababu ya Halmashauri nyingi kushindwa kupanga miradi ya maendeleo na hivyo kusababisha fedha nyingi kurudishwa serikali kuu pale unapofika mwisho wa mwaka wa fedha kwa serikali.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa