Na Elinipa Lupembe
Mkuu wa mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa shule mpya ya sekondari Korongoni kata ya Lemara, mradi unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 400 fedha kutoka serikali kuu.
Mkuu huyu wa mkoa ameuagiza uongozi wa Jiji la Arusha kukamilisha mradi huo kwa kuzingatia kiasi cha fedha kilichotolewa na serikali kwa kuwa fedha za mrdai zimekuja na maelekezo yake.
"Serikali imetoa milioni 400, fedha hizo zitumike kukamilisha mradi kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyoendana na thamani ya fedha, nakemea tabia ya wakurugenzi kuongeza fedha kutoka mapato ya ndani, fedha hizi zikamilishe mradi huu kwa wakati" Amesisitiza Mhe. Mongella.
Aidha amemtaka mhandisi wa Halmashauri hiyo kuzingatia manunuzi ya vifaa vyenye ubora, unaoendana na thamani ya fedha kwa kuwa upatikanaji wa vifaa kwa jiji la Arusha ni rahisi tofauti na halmashauri za pembezoni kama Longido na Ngorongoro hivyo ni muhimu kuonesha utofauti.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Afisa Mtendaji wa katanya Lemara Lucas Nyamhanga, amesema kuwa kiasi hicho cha fedha kitajumuisha ujenzi wa sakafu ya kwanza na ya pili yzenye idadi ya vyumba 8 vya madarasa na matundu 22 ya vyoo.
Amefafanua kuwa lengo la mradi huo ni kuboresha miundombinu ya elimu katika Jiji la Arusha na kupunguza msongamano wa wanafunzi shuleni unaoenda sambamba na ongezeko la wanafunzi linalotokana na Sera ya Elimu bila malipo.
#ArushaFursaLukikuki
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa