Na Elinipa Lupembe
Ule usemi unaosema Kutoa ni moyo na sio utajiri, umejithihirisha leo, kwa Wanachama wa Chama cha Kutetea Haki za Watoto wanaoishi kwenye Makazi mkoa wa Arusha ( ACRO), kwa kukabidhi msaada wa vitu mbalimbali kwa Waathirika wa Maafa ya Katesh wilaya ya Hanang.
Usemi huo umethibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, mara baada ya kukabidhiwa msaada huo, uliotolewa na wanachama hao, ambao wao pia, hushughulika na kusaidia watoto wanaoishi kwenye makao ya kukulea watoto wenye uhitaji.
Mhe. Mongella licha ya kuwashukuru kwa moyo wa utoaji walionao, amekiri kushangazwa na Chama hicho, kutokana na ukweli kuwa, wao pia wanafanya shughuli za kuwasidia jamii yenye uhitaji pia lakini bado wameguswa kutoa kwa wengine wenye uhitaji zaidi.
"Mara nyingi tulizoea wakipita kutaka kushikwa mkono kwa ajili ya kuwasiaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, leo wao wanatoa msaada kwa waathirika wa Maafa ya Katesh, hili jambo limenidhihirishia kweli kutoa sio utajiri bali ni moyo" Amethibitisha Mhe. Mongella.
Aidha amewataka wakazi wa mkoa wa Arusha, watakao guswa kutoa msaada wafanye hivyo, kwa kuwa bado wenzetu wanaKatesh wanahitaji msaada, kazi ya mkoa ni kuratibu na kuhakikisha misaada yote inayotolewa, inawafikia walengwa na si vinginevyo, kama yalivyo maagizo ya Serikali chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
"Tumeelekezwa na Mhe. Rais kuratibu zoezi la upokeaji misaada na kuifikisha kwa waathirika, nitamfikishia salaam za wana ACRO, tendo hili ni funzo kwetu na watanzania wote, tunapaswa kuiga mfano huu, hata hivyo fedha mlizotoa kwa ajili ya kusafirishia mzigo huu, tutaziwasilisha kwa walengwa kwa kuwa hilo ni jukumu la mkoa kusafirisha misaada itakayotolewa kwa waathirika wa Katesh" Amebainisha Mkuu huyo wa mkoa.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Chama cha ACRO, Josephat Mmanyi, amesema wameguswa kutoa msaada wa vifaa hivyo ikiwemo, vyakula, nguo na mashuka, kwa lengo la kuuwasaidia watanzania wenzao wenye shida pamoja na kuunga mkono mhe. Rais Dkt Samia Suluhu pamoja na mkuu wa mkoa wa Arusha.
"Tumeguswa kuwasaidia watu wa Hanang' waliokumbwa na maafa, ili waweze kujiona wapo na ndugu zao, ambao ni sisi watanzania wenzao, tunawaomba wakazi wa Arusha kumuunga mkono mkuu wa mkoa ili wenzetu waweze kupata huduma kama ilivyokuwa awali.
Naye, Afisa Ustawi wa Jamii, Mkoa wa Arusha, Denis Mgie, ameshukuru wadau hao kwa msaada huo kwa kuwa wapo watoto ambao wameathirika katika eneo la Katesh, hivyo msaada huo utakwenda kuwahudumia watoto pia waliokumbwa na maafa hayo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa