Kufuatia taarifa ya matokeo ya Sensa ya wanayamapori, Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Tanzania - TAWIRI, matokeo yameonseha kuwa Tanzania inaongoza kwa kuwa na Simba, Nyati na Chui wengi katika bara la Afrika huku ikishirikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa ya Tembo.
Akiwasilisha Taarifa hiyo Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya utafiti wa wanyamapori kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametangaza rasmi matokeo ya Sensa ya Wanyamapori na kuzindua taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023, kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Gran Melie Aprili 22, 2024.
Sensa hiyo ya wanyamapori imefanywa na TAWIRI kwa kushirikiana na TANAPA, TAWA, NCAA, Idara ya Wanyamapori, na Frankfurt Zoological Society katika mifumo ya ikolojia ya Nyerere-Selous-Mikumi,Saadani-Wamimbiki na Serengeti.
Mkutano huo uliwahusisha wadau wa uhifadhi na utalii, ambapo Mhe. Kairuki amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wanyamapori nchi nzima mapema hapo mwakani.
Aidha, Mhe. Kairuki amesema matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kwenye usimamizi wa wanyamapori nchini na kupanga mipango mbalimbali ya kuboresha uhifadhi na kutangaza utalii duniani.
Mhe. Kairuki ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Serikali ambapo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI) kuandaa mpango kazi kwa ajili ya sensa ijayo huku pia akielekeza watendaji wa wizara yake kuchambua kwa kina matokeo ya sensa hii ili yaweze kuleta tija.
Akitoa taarifa ya sensa hiyo amesema spishi zilizoonyesha idadi kubwa ni pamoja na Nyati (59,878), Tembo (20,006), Nyumbu (19,060), Kongoni (18,361), swalapala (14,031) na Ngiri (13,806), ambapo spishi zilizoonyesha idadi ndogo ni pamoja na Twiga (1,679), Tandala mkubwa/ kudu (1,414) na puku/sheshe (496).
Amefafanua kuwa kwa upande wa Tembo, idadi imeongezeka kutoka 15,501 (2018) hadi 20,006 (2022) na Viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa hadi 0.8% mwaka 2022 ikilinganishwa na 16% wakati wa sensa ya 2018.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa