Katibu Tawala Mkoa wa Arusha ,Missaile Musa amewataka Wakurugenzi wa Halmshauri za Mkoa wa Arusha kubaini makundi au vikundi vinavyojihusisha na uzalishaji wa bidhaa zao ili kupata mafunzo kutoka Tume ya Ushindani (FCC) kwa lengo la kuongeza tija ikiwemo mnyororo wa thamani ,ili kuleta ushindani wa soko.
Agizo hilo limetolewa jana Jijini Arusha na Katibu Tawala,Musa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uhamasishaji wa masuala ya ushindani na Udhibiti wa Bidhaa Bandia kwa wazalishaji Kanda ya Kaskazini.
Alisema endapo vikundi vinavyopewa mikopo na halmashauri vikipata mafunzo ya udhibiti wa ushindani wa kibiashara vitawezesha bidhaa zao kuingia katika masoko kutokana na ubora.
Alisema lengo la kutoa agizo hilo ni kukuza biashara na mnyororo wa thamani ikiwemo udhibiti wa bidhaa bandia na ukaguzi kwa walaji na wauzaji wa bidhaa mbalimbali.
"Wakurugenzi wa Halmshauri shirikianeni na FCC katika kuleta ushindani wa thamani za ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wanaopata mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na halmshauri".
Naye Mkuu wa FCC Kanda ya Kaskazini,Nonge Juma alisema, mafunzo hayo kwa wafanyabiashara wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa yanalengo la kuwezesha kuleta tija katika ushindani wa biashara wanazozalisha ikiwemo kudhibiti bidhaa bandia zisizizosajiliwa na kuleta athari kiuchumi.
Alisisitiza wafanyabiashara hao na wenye viwanda kuhakikisha wanazingatia maadili ya biashara ili kuhakikisha soko linabaki shindani .
Huku Mwenyekiti wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI),Anup Modha alitoa rai kwa wamiliki wa viwanda,wafanyabiashara mbalimbali kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuleta ushindani katika masoko kwa kuzingatia ushindani wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa