Waandishi wa habari zingatieni Sera ya nchi,Sheria na maadili ya uwandishi wa habari katika kutoa taarifa zenu zinazoelimisha jamii ili kukuza uwelewa juu ya mambo ya vijana na wanawake kwa ujumla.
Yamesemwa hayo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega, alipokuwa anafunga mafunzo ya siku mbili ya waandishi wa habari juu ya afya ya uzazi kwa vijana na kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Mafunzo hayo yametolewa chini ya udhamini wa shirika lisilo la kiserikali la Deutsche Stiftung Weltbevolkerung (DSW) kwa lengo la kuongeza uelewa kwa waandishi wa habari katika nyanja ya afya kwa vijana na kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Kwitega amesema kwa Mkoa wa Arusha jumla ya kesi 1437 zilizolipotiwa kati ya mwaka 2017 hadi 2018 juu ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika hospitali zetu na vituo vya polisi.
Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mikakati juu ya afya ya uzazi kwa vijana na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA) ili kujengaTaifa lililo imara kwa ujenzi wa uchumi na Viwanda.
Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la DSW bwana Peter Owaga Ameishukuru Serikali kwa kuonesha ushirikiano wa karibu kwa taasis yake na hivyo kupelekea kazi nyingi kufanyika kirahisi na kuwafikia watu wengi.
Amesema shirika lake linaendelea kutoa mafunzo kwa vijana mbalimbali kutoka katika halmashauri ya Arusha ambao nao wanaporudi kwenye jamii zao huunda vikundi vya kuendelea kusambaza elimu hiyo katika jamii husika, pia wanawapa na mafunzo ya ujasiliamali.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya waandishi wa habari waliopatiawa mafunzo Bi. Mwanaidi Nkwizu amesema wapo tayari kwenda kusambaza elimu waliyopata ili na jamii nayo ipanue uelewa juu ya afya kwa vijana na mpango wa kuthibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Aidha, amemuomba Katibu Tawala kusimamia utaratibu wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali kutoka kwa watumishi wa Serikali ili kurahisha utendaji wao wa kazi.
Mafunzo kwa waandishi wa habari yamefanyika kwa siku mbili na mada mbalimbali zimefundishwa zikiwemo afya ya uzazi wa mpango na mpango wa serikali wa kutihibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa