Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufungua kikaokazi cha Wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wa Taasisi, Mashirika ya umma na wakala za serikali, wanaokutana jijini Arusha kuanzia Agosti 28, 2024 kwenye Kituo cha kimataifa cha Mikutano AICC.
Msajili wa hazina Bw. Nehemia Mchechu mbele ya wanahabari mapema leo Agosti 27, 2024 Jijini Arusha, amesema Mkutano huo utahusisha wenyeviti, wakurugenzi na wakuu wa taasisi waliowekeza kwenye sekta mbalimbali kwa mtaji wa takribani Trilioni 76.
"Ni tukio muhimu sana kwetu kwasababu unakuwa unazungumzia taasisi zote za umma, tunazungumzia kuwakutanisha watu ambao kwa nafasi zao za kuwa Mwenyekiti au Mkurugenzi mkuu ni watu ambao wana nafasi kubwa ya kusimamia uchumi wa nchi yetu." Ameongeza kusema Bw. Nehemia.
Katika hatua nyingine Bw.Mchechu amekiri kuwa Rais Samia Suluhu Hassan kukubali kuwa mgeni rasmi wa Kikao hicho kunaonesha dhamira ya dhati aliyonayo katika maboresho makubwa anayoendelea kuyatekeleza kwenye Taasisi na mashirika hayo akiahidi kuendelea kutekeleza kikamilifu maagizo na maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa