Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella, amepata fursa ya kuzungumza na wanafunzi wa darasa la awali, shule shikizi ya Msingi Kale, kijiji cha Iloirenito Tarafa ya Kitumbeini wilaya ya Longido, alipotembelea shuleni hapo kujionea maendleo ya shule hiyo na mapokezi ya wanafunzi wa madarasa ya awali na la kwanza, leo 30 Januari 2024
Mhe. Mongella licha ya kuridhishwa na uwepo wa wanafunzi shuleni hapo, amewapongeza wanafunzi hao na kuwatakia kila lenye kheri katika safari yao ya masomo, huku akiwasisitiza kutia bidii katika kujifunza ili waweze kuja kulitumikia Taifa lao la Tanzania.
Aidha, amewatia moyo walimu wa shule hiyo licha ya ugumu wa mazingira ya eneo hilo, na kuwasisitiza kuweka juhudi katika kuwafundisha maarifa na stadi zote za maisha ili kupata watalamu wa fani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi hao.
Ameweka wazi kuwa Serikali ya awamu ya sita, imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya elimu, lengo likiwa ni kuhakikisha watoto wote wakitanzania wanapata elimu ili kuzalisha watalamu watakaolitumikia taifa hili katika fani mbalimbali lakini zaidi watoto hao watimize ndoto zao wanazotarajiwa kuwa baada ya kuhitimu masomo yao.
"Kila mtanzania anatambua nia na matamanio ya Mhe. Rais Samia Suluhu, ya kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu karibu na eneo analoishi, ni jukumu lenu walimu na wazazi kushirikiana kuhakikisha lengo lq Serikali linatimia ili kumuunga mkono Rais wetu kwa kazi kubwa anayofanya ikiwa ni pamoja na kuwajali wananchi" Amesema Mhe. Mongella
Mhe. Mongella ametembelea shule hiyo shikizi, ikiwa ni zaiara yake ya kawaida ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ndani ya mkoa wake wa Arusha.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa