Maofisa Watendaji wa Kata Mkoani Arusha, wametakiwa kusimamia vema utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kuhakikisha shughuli zote za maendeleo zinasimamiwa ikiwa ni pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kufanyika kwa vikao na mikutano yote ya kisheria.
Rai hiyo imetolewa wakati wa kikao cha majumuisho, ya ziara ya kawaida ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani Longido, ikiwa ni ufuatiliaji wa utekelezaji wa Ilani ya Chama, iliyofanywa na Kamati ya Siasa Mkoa wa Arusha.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha Thomas Loy Ole Sabaya,
amesisitiza kuwa moja ya jukumu la Maofisa Watendaji hao ni kusimamia miradi yote ya maendeleo inayofanyika katika maeneo yao, ikiwa ni pamoja kushirikisha wananchi kwa kupitia vikao na mikutano ya kisheria ili wananchi wafahamu mambo yanaeyofanywa nra Serikiali ambayo ndio utekelezajiwa Ilani ya CCM.
Komredi Sabaya amesema kuwa, endapo Maofisa Watendaji watatekeleza majukumu yao na kutumiamia njia shirikishi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao, watafikia malengo ya Serikali.
"Wananchi wanatakiwa kufahamu, kiasi cha fedha za miradi zilizoletwa na Serikali katika maeneo yao, zinatekeleza miradi gani, muda wa utekelezaji pamoja na kushiriki hatua zote za utelezaji na mwisho kuwasomea taarifa za mapato na matumizi kwa kila robo kupitia Wenyeviti na Watendaji wa vijiji". Amesema Sabaya
Hata hiyo, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Stephen Ulaya, kufanya msawazisho wa walimu katika shule zote, ili kuwe na uwiano wa walimu na wanafunzi unaoendana na idadi ya shule, hali itakayosaidia shule zote kuwa na walimu watakaowezesha wanafunzi kufundishwa masomo yote.
Katika kikao hicho, Diwani wa Kata ya Matale Lengai ole Nini, amemwomba Mwenyekiti huyo, kuwasaidia kupata walimu sita ili kuwa ni mbadala ya walimu waliohama mfululizo na kuwaacha katika kata hiyo na kusababisha wanafunzi kukosa baadhi ya masomo.
"Walimu sita wamehama katika shule ya msingi Matala, wanafunzi wamebaki hawana walimu hatuwatendei haki, tunaomba walimu wengine mbadala ili kuziba pengo hilo". Amesisitiza Mhe.Ole Nini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John V.K Mongella ameahidi kuchukulia kwa uzito unaostahili hoja ya walimu na kuifanyia kazi huku akikiri kuwa bado kuna upungufu wa walimu kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya shule mpya na kufafanua kuwa licha ya kuwa uhamisho ni haki ya mtumishi ni lazima Maofisa Elimu kufanya kwa umakini mkubwa ili kuhakikikisha shule haikosi walimu.
Mhe. Mongella amemsisitiza Mkuu wa Idara ya Elimu, kupeleka walimu wengine mbadala kweye shule hiyo ili kuziba pengo la walimu hao waliohama kabla ya kufikia tarehe 15, Machi mwaka huu.
Awali Kamati ya siasa imefanya ziara ya siku mbili ya kukagua hali ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 -2025, uliofanyika kwa vitendo kama Mhe. Rais alivyoahidi kuitekeza mara baada ya kuingia madarakani.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa