Wazazi wenye watoto chini ya miaka mitano watakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote ili waweze kupata kinga kamili ya miili yao na kuwajengea afya bora.
Yamesemwa hayo na mratibu wa chanjo Mkoa wa Arusha bwana Azizi Sheshe alipokuwa akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya kampeni shirikishi ya Surua,Rubella na Polio itakayofanyika nchi nzima mapema Octoba.
Amesema kwa mkoa wa Arusha utoaji wa chanjo upo katika hali nzuri japo changamoto kubwa ipo katika utoaji chanjo ya watoto wenye umri wa miezi 18, ambapo wazazi wengi wamekuwa wakiwapeleka watoto wao katika chanjo ya kwanza ya miezi 9 tu.
“Wazazi wengi wamekuwa wakipuuzia chanjo ya pili ya miezi 18 kwa watoto na hali hii imepelekea watoto wengi kutokuwa na kinga kamili ya miili yao”.
Kutokana na changamoto hii ndio maana serikali imeamua kufanya kampeni hii nchi nzima ili kuhamasisha watoto wote waweze kupatiwa chanjo ya Surua, Rubella na Polio ili kuwaongezea kinga kamili katika miili yao.
Amesisitiza kuwa katika kampeni hii ambayo hata katika mkoa wa Arusha itafanyika na walengwa ni watoto wote walio chini ya miaka mitano na watapatiwa chanjo hiyo katika vituo mbalimbali vilivyoainishwa kwenye makazi ya watu.
Amewataka wazazi wote kuhakikisha watoto wao walio chini ya miaka mitano wanapatiwa chanjo hiyo hata kama alishapata zote mwanzo anaruhusiwa kurudia ili kumuweka katika nafasi nzuri zaidi ya kuongeza kinga ya mwili.
Amesema ugonjwa wa Surua na Rubella yanaenezwa kawa njia ya hewa hasa kwa kukohoa au kupiga chafya na ni magonjwa yanayoenea kwa kasi sana,wakati ugonjwa wa Polio unaenezwa kwa njia ya ulaji chakula kichafu au maji yaliyochafuliwa.
Bwana Sheshe amesema adhari za ugonjwa wa Surua kwa mtoto ni; masikio kutoa usaha, kupata vidonda vya macho,Nimonia, Utapiamlo, kuvimba ubongo na hata kupelekea kifo na Rubella madhara yake kwa mtoto ni kupata mtoto wa jicho, matatizo ya Moyo, Kutosikia vizuri, mtindio wa ubongo na matatizo ya ukuaji wa mwili.
Hivyo amewasisitiza wazazi wote wawapeleke watoto wao katika vituo vya kupatiwa chanjo ili kuwaongezea kinga ya mwili watoto wao na kuwaepusha na magonjwa mbalimbali yanayoweza kuwapata.
Dokta Thomas Lyimo mwakilishi kutoka UNICEF,amesema taasis yake inashirikiana vyema na serikali kwa kuhakikisha chanjo zinapatikana nchini kwa wingi na kwa wakati na amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi kuwapatia chanjo watoto wao.
Kampeni shirikishi ya Surua na Rubella kwa Mkoa wa Arusha itaanza rasmi Octoba 17 hadi Octoba 21 katika vituo mbalimbali vilivyoainishwa na chanjo hiyo itatolewa bure na kwa mfumo wa sindano,hivyo wazazi wanatakiwa kuhakikisha watoto wao wenye umri chini ya miaka mitano wanapatiwa chanjo hiyo.
Hatimiliki ©2018 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Haki Zote Zimehifadhiwa