Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda Leo Jumamosi Septemba 28, 2024 amekutana na kuzungumza na Msanii maarufu wa sanaa ya maigizo na vichekesho kutoka nchini Kenya Bw. Daniel Ndambuki maarufu kama Churchil ambapo wamekubaliana kushirikana katika Programu maalum ya kuinua sanaa ya Uigizaji na Vichekesho Mkoani Arusha.
Churchil ambaye pia ni Mtangazaji wa kipindi cha Runinga cha Churchil Show amefanya kazi kwenye tasnia ya Vichekesho tangu mwaka 1996 na jukwaa lake la Churchil show limetoa fursa kwa mamia ya Vijana kuweza kuonesha vipaji vyao, akisifika pia kwa kugundua na kukuza vipaji vya vijana wengi wa pembe ya Afrika Mashariki kupitia program zake kadhaa za kukuza vipaji ikiwemo ya "Top Comic" inayojumuisha wataalamu wa kunoa vipaji zaidi ya 20.
Mhe. Makonda kando ya kutangaza Onesho kubwa Jijini Arusha la Churchil Show mwezi Disemba mwaka huu, amewaambia wanahabari kuwa dhamira yake mara zote ni kuhakikisha wananchi wa Arusha wanastawi kiuchumi kupitia vipaji vyao, akiahidi kuendelea kubuni na kufungua fursa zaidi kwa Kila mwananchi wa Arusha ili kuweza kunufaika na uwepo wake kama Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
" Kila mtu Mungu amempa kitu cha tofauti na sisi kama sehemu ya serikali ya Mkoa jukumu letu ni kuhakikisha tunatengeneza mazingira mazuri ya vijana wa mkoa wetu kuhakikisha wanatumia vipaji vyao kutengeneza maisha yao na uchumi wao. Churchil Show ni moja ya Programu kubwa Afrika na duniani na ni programu ambayo inabadilisha maisha na kukuza vipaji vya vijana wengi na sasa ni zamu ya wananchi wa Arusha", Amesema Mhe. Makonda.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.