Naibu Waziri wa madini Mhe. Steven Kiruswa amewataka wafanyabiashara ya madini wa kati kufuata sheria zilizowekwa katika masoko ya madini.
Ameyasema hayo alipokuwa akifunga kikao cha siku 2 cha chama cha wafanyabiashara wa kati wa madini nchini (CHAMMATA) kilichofanyika Jijini Arusha.
Amesema serikali ipo tayari kushirikiana na chama hicho kama inavyoshirikiana na vyama vingine katika sekta hiyo ya madini ili changamoto zao ziweze kutatuliwa kwa pamoja.
Amesisitiza kuwa sekta ya madini inamchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi kwani kwa mwaka 2020/2021 Serikali ilikusanya kiasi cha sh. bilioni 584 na malengo ya makusanyo kwa mwaka 2022/2023 ni bilioni 822.
Madini ni kitega uchumi kikubwa cha nchi hivyo wafanyabiashara wote wakubwa, wakati na wadogo wafuata sheria za uuzaji wa madini katika masoko na vituo vya kuuzia madini.
Akisisitiza zaidi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe.John Mongella Mkuu wa Wilaya ya Longido Mhe.Nurdin Babu amewataka wafanyabiashara wa madini kufuata sheria za madini hasa za uuzaji ili kukuza pato la Taifa.
Nae, mwenyekiti wa CHAMMATA bwana Jeremiah Kipuyo amesema wao kama wafanyabiashara wa kati wa madini wanaunga mkono Serikali katika kuuza madini kwenye masoko ili kuyalinda na kukuza pato la taifa.
Amesema kuanzishwa kwa chama hicho kutasaidia kufanya kazi kwa karibu na Serikali na kupiga vita utoroshaji wa madini kiholela na kuzuia uingizaji wa madini feki katika soko.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara ya madini (TAMIDA) bwana Sammy Mollel amewataka wafanyabiashara wa kati wa madini wakafanye biashara zao katika masoko yaliyotengwa na Serikali ili kudhibiti wizi wa madini na upotevu wa kodi kwa Serikali.
Pia, ameiyomba serikali kutowazuia wafanyabiashara hao kuuza madini ndani ya Mikoa yao tu badala yake wauze hata nje ya Mikoa yao kwa kufuata sheria za masoko husika.
Katika kikao hicho Mhe. Kiruswa amezindua Katiba ya chama hicho kama ishara ya kutambulika na Serikali na kuweza kuanza kazi zao rasmi.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.