Taasisi na mashirika ya Umma nchini Tanzania yametakiwa kuanza kufikiri kuhusu uwekezaji nje ya nchi kama sehemu ya kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Msajili wa Hazina Bw. Nehemia Mchechu ametoa wito huo mapema leo Agosti 27, 2024 mbele ya wanahabari Jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumzia ujumbe wa mwaka huu wa Kikaokazi cha wakuu wa Taasisi, mashirika na wakala za serikali, kikao kinachotarajiwa kufunguliwa Jumatano hii na Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.
"Kikao cha mwaka huu kimejikita katika kuzisukuma Taasisi za umma na mashirika ya umma kuanza kufikiria uwekezaji nje ya mipaka ya Tanzania, tunataka Taasisi zetu ziwe na mawazo mapana ya kufikiri nje ya mipaka na dhamira hiyo ili itimie lazima tuanze kubadilika kwenye utendaji wetu wa kazi." Amesema Msajili wa Hazina.
Nehemia Mchechu akitolea mfano wa Taasisi zenye sifa ya kuwekeza nje ya nchi, amezitaja Taasisi za mfano kuwa ni Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete, Shirika la Reli Tanzania, Shirika la ugavi Tanesco na Shirika la ndege ATCL akiwataka kufikiri namna wanavyoweza kutoka nje na kutoa huduma nje ya Tanzania.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.