“Tutamtumia mrembo wa Dunia katika kutangaza utalii wa nchi yetu ili Dunia nzima ijue Tanzania kuna vivutio vizuri vya utalii ambavyo vitavuta watalii wengi kuja nchini kwetu”.
Yamesemwa hayo na waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Dokta Harrison Mwakyembe, alipokuwa akizungumza na mrembo wa Dunia Bi. Vanessa Ponce alipotembelea shule ya sekondari Moshono iliyopo jijini Arusha na kugawa taulo za kike mapema wiki hii.
Mwakyembe amesema, atazungumza na waziri wa maliasili na utalii ili kumuwezesha mrembo huyo wa dunia kupata nafasi ya kutembelea mbunga mbalimbali za nchi na kuleta hamasa hata kwa wageni wengine kutembelea hifadhi zetu.
Amesema, mbali na kampeni hiyo ya ugawaji wa taulo za kike uliofanywa na mrembo huyo wa dunia bado wanaweza kumtumia katika kutangaza utalii wa nchi kwani dunia nzima wanafahamu yupo Tanzania kwa sasa,hivyo ni fursa nzuri kwa nchi kuona namna ya kumtumia kutangaza hifadhi zetu.
Amesisitiza zaidi kuwa serikali inaendelea na mpango wake wakutangaza utalii pande zote za dunia ili kuongeza mapato ya nchi na kuipeleka nchi katika uchumi wa kati yani uchumi wa viwanda.
Nae Mkurugenzi mwendeshaji wa mashindano ya urembo Tanzania Basilla Mwanukuzi, amesema wanashirikiana na uongozi wa urembo duniani katika kufanya kazi mbalimbali za kijamii ilikuleta hamasa zaidi kwa watu hapa nchini.
Mrembo wa dunia yupo nchini kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kwa kushirikiana na mrembo wa Tanzania Sylivia Sebastian ili kuleta hamasa kwa jamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.