OR-TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu Atupele Mwambene amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la ubainishaji wa Watoto wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha wanaandikishwa shule na kupatiwa afua stahiki kulingana na mahitaji waliyonayo.
Ameyasema hayo leo Septemba 20,2025 wakati wa ufungaji wa Maadhimisho ya miaka 30 ya Elimu Jumuishi uliofanyika katika shule ya Sekondari Maalum Patand, Jijini Arusha
Amesema zoezi la ubainishaji wa watoto wenye Mahitaji maalum litafanyika kwa kushirikisha kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na watendaji waliopo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha hakuna mtoto anayefichwa.
Mwambene anafafanua kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi, walimu na shule Jumuishi kwa ujumla ikiwemo uongezaji wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Aidha, amewataka washirika wa maendeleo kuwekeza nguvu zaidi katika eneo la Elimu Jumuishi ili kwenda sambamba na mahitaji ya dunia yanayomtaka kila mtoto kupata elimu.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.