Na. James K. Mwanamyoto OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa mwezi mmoja kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule mpya za sekondari za bweni za wasichana za mikoa ambazo zimejengwa katika halmashauri zao ili wanafunzi walioripoti katika shule hizo wapate mazingira bora na rafiki ya kupata elimu.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati akipokea taarifa za ujenzi wa shule hizo 26 za sekondari za wasichana za mikoa wakati wa kikao cha tathmini ya ujenzi wa shule hizo kilichofanyika katika Ukumbi wa Arnautoglo wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mchengerwa amesema, alitegemea wakurugenzi watoe taarifa ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hizo kwa asilimia 100 jambo ambalo halijatekelezeka, wakati yeye akiwa kwenye ziara ya Mhe. Rais Mkoani Rukwa alimuahidi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ndani ya mwezi mmoja miundombinu ya shule zote 26 itakuwa imekamilika.
Waziri Mchengerwa ameanisha kuwa, wapo wakurugenzi amewapatia wiki mbili, wiki tatu na wengine mwezi mmoja wa kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa miundombinu iliyosalia katika shule hizo za wasichana za mikoa, isipokuwa mkurugenzi anayesimamia ujenzi wa shule ya mkoa wa Rukwa ambaye amempatia miezi 2.
“Hakutakuwa na nyongeza ya muda katika kipindi ambacho tumekubaliana mkamilishe ujenzi wa miundombinu ya shule hizo, na sitosita kumchukulia hatua mkurugenzi yeyote atakayeshindwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule kwa mujibu wa makubaliano yetu,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa, yeye binafsi pamoja na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wanawategemea wakurugenzi hao katika usimamizi wa miradi mbalimbali inayolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Bw. Kagurumjuli Titus amesema kwamba wamepokea maelekezo ya Waziri Mchengerwa na kuhaidi kuwa, manispaa yake itakamilisha ndani ya siku 15 hadi 21 ujenzi wa miundombinu ya shule ya mkoa ya Dar es Salaam ambayo ilikuwa haijakamilika.
rc_mkoa_arusha-20240817-0014.jpg9
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.