Wazazi na walezi wametakiwa kuachana na dhana potofu, badala yake, kuwapeleka watoto wenye umri wa miezi tisa mpaka miaka mitano, kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio, Surua-Rubela kwa kuwa chanjo hizo zinaokoa maisha ya watoto pamoja na kuokoa gharama kubwa ,ambazo familia na taifa ingezitumia kwa kutibu magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa kinga chanjo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya kitaifa ya Chanjo kimkoa, uzinduzi uliofanyika, kwenye kituo cha Afya cha Nduruma, Halmashauri ya Arusha, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, amesema kuwa, lengo la kampeni ya chanjo kitaifa ni kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto, pamoja na kuokoa gharama za kubwa za matibabu kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika kupitia chanjo.
Katibu Tawala huyo, ameendelea kufafanua kuwa, tafiti zinaonesha kuwa, hadi kufikia mwaka 2019, magonjwa yanayokingika kwa chanjo yameendelea kuongezeka, kutoka magonjwa manne mpaka kufikia magonjwa 13, hivyo ni vyema kuchukua tahadhari na kuwataka wazazi kuhakikisha watoto wamepata chanjo zote muhimu, sambamba na kuwaongezea kinga zaidi, wakati zoezi la chanjo kitaifa linapojitokeza kama sasa.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo, amesema kuwa, licha ya changamoto za umbali wa vituo vya kutolea huduma za afya, bado halmshauri zinaendelea kutoa huduma za mikoba kwa kuwafuata wananchi kokote walipo, huku Serikali ya awamu ya tano ikiwekeza fedha nyingi kwenye ujenzi wa vituo vya afya nchini, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za afya ndani ya maeneo yao wanayoishi .
Awali, Katibu Tawala wilaya ya Arumeru, mwalimu James Nchembe, amesisitiza kuwa, chanjo hizo zinatolewa bure, na zinatolewa kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za afya ndani ya wilaya hiyo, hivyo ni vema kila mzazi kutenga saa chache kumpeleka mtoto wake kupata chanjo hizo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Arusha, Alvera Ndabagoye, ameisisitiza kuwa, ubora wa chanjo hizo, umethibitishwa kwa viwango vya kimataifa, hivyo ni vyema wazazi na walezi kupuuzia maneno ya uzushi dhidi ya chanjo hizo, na kuwapeleka watoto wa umri huo kupata chanjo hizo muhimu.
Ameongeza kuwa serikali inafanya kampeni ya kitaifa ya chanjo za Polio na Surua-Rubela, ikiwa na mkakati wa kuwa na taifa lenye watoto wasiosumbuliwa na maradhi, ikiwemo matatizo ya moyo, mtindio wa ubongo, upofu wala wenye kupooza viuno vya mwili.
Katika hali isiyotarajiwa mamia ya wazazi na walezi wamejitokeza kwa wingi, kwenye kituo cha Afya Nduruma, wakiwa wamembatana na watoto wao wenye umri wa kuanzia miezi 9 Hadi miaka 5, ili kupata chanjo hizo, huku wengi wao wakiipongeza serikali ya awamu ya tano, kwa kujali afya za wananchi wake, hasa waishio vijijini kama wao.
Leila Mohammed mkazi wa Kijiji cha Nduruma Kati, ameishukuru Serikali kwa kuleta chanjo hizo muhimu kwa watoto wao, na kuongeza kuwa Serikali imewapa elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa chanjo hizo, jambo lililosababisha wazazi hao, kujitokeza kwa wingi kuwaleta watoto wao.
"Tumeelimishwa vya kutosha, umuhimu wa chanjo hizi, chanjo zinazuia magonjwa ya moyo, macho, ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo, imetulazimu kuwaleta watoto wetu, kwani hakuna mzazi anayependa mtoto wake apate matatizo" amesema Leila.
Mkoa wa Arusha umezindua rasmi kampeni ya utoaji chanjo ya Surua,Rubella na Polia kwa watoto kuanzia miezi 9 hado miaka mitano na kampeni hii itadumu kwa siku 5 kuanzia Octoba 17 hadi Octoba 21.
Copyright ©2017 Arusha Regional Comissioner's Office. All rights reserved.